Featured Kitaifa

SPIKA WA BUNGE LA TANZANIA ATETA NA KATIBU MKUU MPYA WA FP-ICGLR

Written by mzalendoeditor

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Mhe. Dkt. Tulia Ackson, leo tarehe 8 Mei 2025, amemkaribisha na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Jukwaa la Mabunge ya Nchi Wanachama wa Mkutano wa Kimataifa wa Ukanda wa Maziwa Makuu (FP-ICGLR), Dkt. Deo Mwapinga, Ofisini kwake Bungeni, Dodoma.

Katika mazungumzo hayo, Mhe. Dkt. Tulia Ackson amempongeza Dkt. Mwapinga kwa kuchaguliwa katika wadhifa huo muhimu, na amemhakikishia ushirikiano wa dhati kutoka Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika utekelezaji wa majukumu yake mapya ya kuliongoza Jukwaa hilo. Aidha, amesisitiza dhamira ya Tanzania kuendelea kushirikiana na taasisi za kikanda katika kukuza demokrasia, utawala bora na maendeleo endelevu.

Dkt. Mwapinga alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Jukwaa hilo, tarehe 25 Aprili, 2025 katika kikao cha juu cha Maspika wa Mabunge ambayo ni Wanachana wa Jukwaa hilo kilichofanyika Luanda, Angola. Ataongoza taasisi hiyo kwa kipindi cha miaka mitatu (3), kwa mujibu wa Katiba ya Jukwaa, ikiwa ni nafasi inayoweza kurejewa (re-election) kwa mujibu wa taratibu.

About the author

mzalendoeditor