Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Selemani Jafo (Mb), ametoa rai Wazalishaji wa ndani kuongeza uzalishaji wa mafuta ya kula ili kupunguza uagizwaji wa bidhaa hiyo kutoka nje ya nchi, kwa lengo la kulinda viwanda vya ndani na ajira za Watanzania.
Vilevile Dkt Jafo amebainisha kuwa Serikali iko tayari kuwasaidia wadau wanaotaka kuwekeza katika viwanda hususani viwanda vya uchakataji mafuta ya kula
Akizungumza wakati wa ziara yake katika Kiwanda cha Mafuta cha Sunshine kilichopo Zuzu Jijini Dodoma Aprili 23,2025, Dkt. Jafo amesema kuwa hakuna sababu kwa Watanzania kuendelea kutegemea mafuta kutoka nje ya nchi wakati uwezo wa kuzalisha upo.
“Watanzania sasa kuna kila sababu ya kujivunia vya kwetu. Tutumie bidhaa zetu. Tukizalisha kwa wingi tutakidhi mahitaji ya ndani na kupunguza matumizi ya fedha za kigeni ambazo zimekuwa zikitetemesha uchumi wa nchi,” amesema Dkt. Jafo.
Vilevile Dkt Jafi amebainisha kuwa Serikali imefanya uwekezaji kwenye kilimo cha mazao ya kuzalisha mafuta na kuwa ni imani yake kuwa muda mfupi ujao Tanzania haitakuwa na haja ya kuagiza mafuta ya kula kutoka nje.
Kwa upande wake, Afisa Biashara kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Bw. Amri Kibwana, aliwataka wakazi wa Mkoa huo kuendelea kutumia bidhaa zinazozalishwa na viwanda vya ndani ili kuchochea ukuaji wa uchumi wa Mkoa na Taifa kwa ujumla.
Naye Meneja Uzalishaji wa Kiwanda cha Sunshine, Bw. Athumani Omary, aliiomba Serikali kuwalinda Wazalishaji wa ndani kwa kudhibiti uingizwaji wa mafuta kutoka nje, akisema hali hiyo inaathiri ukuaji wa viwanda vya ndani.
“Tunaomba Serikali ituangalie kama wazalishaji wa ndani. Uingizwaji wa mafuta kutoka nje unaua viwanda vya ndani na kupunguza ajira,” amesema Omary.