Featured Kitaifa

TAWIRI YAGUNDUA DAWA YA ASILI YA KUOTESHA NYWELE NA KUZUIA NYWELE KUKATIKA

Written by mzalendoeditor

 

Taasisi  ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania(TAWIRI) imegundua dawa ya kuotesha nywele au kuzuia nywele kutoka kwa binadamu kutokana na mimea inayotumika kama tiba asili ugunduzi huo ulianza  mwaka 2013 na kukamilika mwaka huu katika mimea inayotumika kwa tiba asili katika ukanda wa kaskazini mwa Tanzania katika wilaya za Ngorongoro, Mbulu na Hanang kwa watu jamii ya Masai, Hadzabe, Datoga na Iraqw.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Jijini Arusha kuhusu ugunduzi wa dawa ya kuotesha nywele au kuzuia nywele kutoka kwa kutumia mmea uitwao Mporojo, Mkurugenzi wa Utafiti kutoka TAWIRI, Dkt, Julius Keyyu amesema taasisi hiyo imefanya utafiti kwa kipindi cha miaka 12 na hatimaye imepata dawa hiyo ya watu wenye changamoto za vipara pamoja na nywele kutokuota

Dk, Keyyu alisema mmea huo kwa kiingereza unaitwa wormwood albizia, bitter false thorn, jina la kisayansi unaitwa Albiziaanthelmintica na kwa Kimasai unaitwa Ormuktan ambapo wamasai wanatumia magome na mizizi yake kutibu minyoo, malaria na maumivu ya miguu, mgongo na misuli.

Alisema Utafiti huu ulikwenda zaidi ya matumizi haya na kugundua uwezo wa mmea huu kuotesha nywele au kuzuia nywele kutoka na tayari umepata hati miliki (Hataza) hii inaitwa ‘Composition for Hair Growth Stimulation or Hair Loss Prevention Using an Extract of Albizia anthelmintica’.

Alisema Tawiri ni taasisi ya wanyamapori lakini pia inapofanya tafiti hizo inakwenda sanjari na mimea na ndio maana wamebaini mmea huo wa Mporojo unasaidia nywele kuota na kukua zaidi kwa wale wenye changamoto za kutokuota nywele kwa wanawake na wanaume

Alisema gharama yake ni kwa shampoo ni sh, 31,000 na sh, 75,000 mafuta sawa na dola12  kwa shampoo na dola 24 kwa mafuta kwa jumla na upande wa rejareja ni sh, 76,000 kwa shampoo na sh, 152,000 kwa mafuta endapo wakipata mawakala wa ndani na nje ya nchi baada kusaini mkataba wa makubaliano kati ya TAWIRI na mawakala.

Alisema teknolojia ya Hataza hii imetolewa (patent transfer) kwa kampuni ya Winwik Enterprise co. ltd ya Korea Kusini ambayo ni watengenezaji wa Kimataifa wa dawa na vipodozi.

“Tayari kampuni hii imeshatengeneza dawa ya kuotesha nywele (Albizia Hair Loss Care) katika mfumo wa Shampoo (shampuu ya wanawake na wanaume), Dawa(Treatment), na Mafuta (Hair Essence Tonic),Dawa/ vipodozi hivi vitaanza kupatikana kwa bei ya jumla kwa mawakala na pia rejareja hivi karibuni.”

Alisema utafiti wa jinsi ya kuotesha Mporojo (propagation) kwa ajili ya kilimo umeanza ili kuzuia mmea huu kutoweka kutokana na uvunaji wa magome kutoka mimea iliyopo porini

Alisema lengo la  utafiti huo lilikuwa kufanya ugunduzi wa dawa na vipodozi kutokana na bioanuwai ya mimea inayotumika kwa tiba asili na pia kubaini mimea inayotumika kwa tiba asili ambayo iko katika hatari ya kutoweka ili kuihifadhi katika bustani za mimea au ‘botanical garden’.

Alisema kutokana na utafiti wa bioanuwai ya mimea inayotumika kwa tiba asili, watafiti wa Tawiri  wamepata Hataza  tatu za ugunduzi wa dawa au vipodozi asili ambazo ni  dawa hiyo ya kuotesha nywele au kuzuia nywele kutoka kwa kutumia mmea uitwao Mporojo Alisema dawa ya  ya kuotesha nywele (Albizia Hair Loss Care) imetengenezwa katika mfumo wa shampoo (shampuu ya wanawake na wanaume), dawa (Treatment), na Mafuta (Hair Essence Tonic).

Alisema dawa na vipodozi hivyo vitaanza kupatikana kw bei ya jumla kwa mawakala na pia rejareja hivi karibuni kwanni dawa au vipodozi hivi vinatumika kuotesha nywele, kuboresha,  kuimarisha nywele (zisikatike, kuwa nyingi), kuzuia nywele kutoka (kuzuia kipara), au kuondoa kipara.

Aidha, kutokana na utafiti huo, taasisi hiyo pia imepata hataza  nyingine mbili kutokana na bioanuwai ya mimea inayotumika kwa tiba asili ambazo ni ugunduzi wa kipodozi cha kung’arisha ngozi na kuondoa makunyanzi kwa kutumia mmea wa Mugufe.

Alisema Mmea huo kwa kiingereza unaitwa Evergreen shrub,blue bush cherry, na kwa jina la jina la kisayansi la mmea huu unaitwa Maerua edulis ambapo mmea huu kwa Kidatoga unaitwa Ekwida na jamii hii inatumia majani yake kutibu minyoo, tumbo na ngiri

Alisema utafiti huo ulikwenda zaidi ya matumizi haya na kugundua uwezo wa mmea huu  katika kung’arisha ngozi na kuondoa makunyanzi na kuongeza kuwa

Teknolojia ya hataza hii bado haijanunuliwa au kupewa kampuni yoyote, hivyo bado taasisi na washirika wake wanaendelea kuitangaza ili kupata  atakayeihitaji ili kutengeneza kipodozi cha kung’arisha ngozi na kuondoa makunyanzi.

Pia wamegundua dawa nyingine ya tatu ambayo ni dawa ya kuotesha nywele au kuzuia nywele kutoka kwa kutumia mmea uitwao Chimbulei (Kigwala, Mphata na kuongeza kuwa mmea huo kwa kiingereza unaitwa Apple leat, broadlance-pod na kwa jina la kisayansi unaitwa Lonchocarpus eriocalyx.

Alisema mmea huo kwa Kisonjo unaitwa Ekurehe ambapo Wasonjo wanatumia magome na mizizi yake kutibu kikohozi na mafua kwani utafiti huu ulikwenda zaidi ya matumizi hayo na kugundua uwezo wa mmea huu kuotesha nywele au kuzuia nywele kutoka.

Kwamujibu wa Dk, Keyyu alisema teknolojia  hiyo bado haijapewa kampuni yoyote, hivyo bado taasisi na washirika wake wanaendelea kuitangaza ili kupata atakayeihitaji ili kutengeneza dawa ya kuotesha nywele au kuzuia nywele kutoka.

Wakati huo huo, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Tawiri, Rogastian Msafiri alisisitiza utafiti huo ni nyota njema kwa nchi ya Tanzania katika kuhakikisha ataza mbalimbali zinalindwa ili kuhakikisha mimea asil8 inatunzwa na watafiti kufanya tafiti mbalimbali na kuja na matumaini mengine kwa jamii na wanyamapori.

About the author

mzalendoeditor