Featured Kitaifa

AWAMU YA PILI UBORESHAJI, UWEKEKAJI WAZI WA DAFTARI LA WAPIGA KURA KUANZA MEI

Written by mzalendo

Na. Mwandishi Wetu, Dodoma 

Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura awamu ya pili utafanyika sambamba na uwekaji wazi wa Daftari la Awali la Wapiga Kura kuanzia tarehe 01 Mei, 2025 na kukamilika tarehe 04 Julai, 2025.

Akizungumza jijini Dodoma leo tarehe 14 Aprili, 2025 Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Rufani, Mhe. Jacobs Mwambegele amesema zoezi la uboreshaji wa Daftari litafanyika kwa mizunguko mitatu ambapo mzunguko wa kwanza utajumuisha mikoa 15, mzunguko wa pili mikao 16 na mzunguko wa tatu utajumuisha vituo vya magereza na vyuo vya mafunzo.

Ameitaja mikoa itakayohusika kwenye mzunguko wa kwanza wa uboreshaji kuwa ni pamoja na Geita, Kagera, Mara, Shinyanga, Mwanza, Simiyu, Rukwa, Tabora, Katavi, Kigoma, Iringa, Ruvuma, Mbeya, Njombe na Songwe ambapo zoezi hilo litafanyika tarehe 01 hadi 07 Mei, 2025.

Mikoa ya mzunguko wa pili ni pamoja na Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Tanga, Morogoro, Pwani, Singida, Dodoma, Dar es Salaam, Lindi, Mtwara, Mjini Magharibi, Kaskazini Unguja, Kusini Unguja, Kaskazini Pemba na Kusini Pemba ambapo zoezi hilo litafanyika tarehe 16 hadi 22 Mei, 2025.

“Mzunguko wa tatu wa zoezi la uboreshaji wa Daftari utahusisha vituo 130 vilivyopo kwenye magereza ya Tanzania Bara na vituo 10 vilivyopo katika Vyuo vya Mafunzo Tanzania Zanzibar kwa wakati mmoja na utafanyika kwa muda wa siku saba kuanzia tarehe 28 Juni, 2025 hadi tarehe 04 Julai, 2025,” amesema Jaji Mwambegele.

Ameongeza kuwa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa awamu ya pili, utafanyika ngazi ya kata kwa Tanzania Bara na ngazi ya jimbo kwa Tanzania Zanzibar, ambapo jumla ya vituo 7,869 vitahusika, vituo 7,659 vipo Tanzania Bara na vituo 210 vipo Tanzania Zanzibar.

“Tunatarajia kuwa katika awamu ya pili ya uboreshaji, wapiga kura wapya 1,396,609 wataandikishwa, wapiga kura 1,092,383 wataboresha taarifa zao na wapiga kura 148,624 watafutwa kwenye Daftari kwa kukosa sifa za kuendelea kuwepo kwenye Daftari,” amesema Jaji Mwambegele.

Amesema zoezi hilo linafanyika kwa mujibu wa masharti ya kifungu cha 16(5) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya mwaka 2024 kinachoipa Tume jukumu la kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mara mbili mara baada ya uchaguzi mkuu na kabla ya uteuzi wa wagombea kwa uchaguzi mkuu unaofuata.

Amesema zoezi hilo litahusisha kuandikisha wapiga kura wapya ambao ni raia wa Tanzania wenye umri wa miaka 18 na zaidi na watakaotimiza umri huo ifikapo tarehe ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, kutoa kadi mpya kwa wapiga kura waliopoteza kadi au kadi zao kuharibika na kutoa fursa kwa wapiga kura walioandikishwa kurekebisha taarifa zao yakiwemo majina na taarifa nyingine;

Mambo mengine ni kuhamisha taarifa za wapiga kura waliohama kutoka kata au jimbo walipoandikishwa awali na kuondoa taarifa za wapiga kura waliopoteza sifa za kuwemo kwenye Daftari kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kifo.

Wakati huohuo, Jaji Mwambegele amesema kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 11(1) na (2) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024, Tume pia ina jukumu la kuandaa Daftari la Awali la Wapiga Kura na kuliweka wazi kwa umma.

Amesema lengo la uwekaji wazi wa Daftari hilo ni kutoa fursa kwa wananchi kukagua, kufanya marekebisho ya taarifa za wapiga kura na uwekaji wa pingamizi dhidi ya wapiga kura waliomo kwenye daftari ambao hawana sifa.

“Daftari la Awali la Wapiga Kura litabandikwa katika vituo vyote vilivyotumika wakati wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura awamu ya kwanza. Zoezi hili la uwekaji wazi wa Daftari la Awali la Wapiga Kura litafanyika pamoja na uboreshaji wa Daftari wa awamu ya pili,” amesema.

Tume iliboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura awamu ya kwanza kuanzia tarehe 20 Julai, 2024 na kukamilisha tarehe 25 Machi, 2025.
Mwisho.

About the author

mzalendo