Featured Kitaifa

VIJANA WANAOPATA VVU NI TAKRIBANI 34.3% – MAJALIWA

Written by mzalendo
Na Gideon Gregory, Dodoma 
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa ametoa rai kwa Watanzania kuendelea kuchukua tahadhari kwa kuwa ugonjwa wa UKIMWI bado ni tishio na kuongeza kuwa kiwango cha maambukizi mapya ni watu 60,000 kila mwaka ambapo vijana wanaopata VVU maambukizi ni takribani asilimia 34.3 ya maambukizi mapya. 
Waziri Mkuu ametoa rai hiyo leo Aprili 9,2025 Bungeni Jijini Dodoma wakati akisoma hotuba ya bajeti ya bajeti ya ofisi yake kwa mwaka wa fedha 2025/26 na kuongeza kuwa Serikali itaendelea kuratibu shughuli za UKIMWI kwa kutoa huduma endelevu na stahimilivu kwa WAVIU.
“Serikali itaendelea kuimarisha Mfuko wa Udhamini wa UKIMWI ili uweze kufanikisha malengo ya nchi katika kutokomeza UKIMWI ifikapo 2030, kuweka msukumo katika kupunguza maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto,kuhamasisha mabadiliko ya tabia katika jamii ili kupunguza maambukizi mapya ya VVU,”amesema. 
Sambamba na hayo, amesema Serikali inatambua mabadiliko ya sera za misaada kutoka kwa baadhi ya wafadhili wa muda mrefu wa masuala ya UKIMWI hivyo kufuatia mabadiliko hayo, Serikali inachukua hatua madhubuti kwa kushirikiana na sekta binafsi katika kuimarisha uwekezaji kwenye eneo la utaoji huduma kwa WAVIU. 
“Hatua hizo zenye lengo la kuwezesha Taifa 
letu kujitegemea zitaendelea kuchukuliwa pia katika maeneo mengine, niwahakikishie Watanzania wote, kuwa, Serikali itaendelea kuhakikisha huduma zinazohusiana na masuala ya UKIMWI zinaendelea kupatikana na hakuna Mtanzania atakayekosa huduma hizo,”amesema. 

About the author

mzalendo