Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe,akipata maelezo mara baada ya kutembelea kiwanda Cha Chai Cha Mufindi kinachoendeshwa na kampuni ya DL kutoka Nchini Kenya,wakati wa ziara yake Mkoani Iringa
…..
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe (Mb) ameuagiza uongozi wa kiwanda Cha Chai Cha Mufindi kinachoendeshwa na kampuni ya DL kutoka Nchini Kenya kuhakikisha wanalipa stahiki za wafanyakazi pamoja na wakulima wadogo wadogo kabla ya mwaka wa fedha 2024/2025 kuisha.
Mhe. Kigahe ametoa agizo hilo wakati wa ziara alipotembelea kiwanda hicho kilichopo Kijiji Cha Itona Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa
Mhe. Kigahe amesema kuwa uongozi unatakiwa kuwalipa wafanyakazi hao mishahara ya miezi mitatu pamoja na kuwalipa wakulima wadogo wanaoidai kampuni hiyo zaidi ya milioni 200. Hivyo waanze kuwalipa kabla ya kuisha kwa mwezi wa sita mwaka huu 2025.
Adha, ameongeza kwa kusema kuwa pamoja na changamoto zilizopo kiwandani hapo lakini wanatakiwa walipe madeni hayo ambapo wafanyakazi na wakulima wanadai milioni 124, mafao kwa wastaafu yanayodaiwa ni Shilingi bilioni 1.6 na Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi inadai Shilingi milioni 78 za ushuru wa huduma japo kwa sasa wametakiwa kuanza kuwalipa kwanza wafanyakazi na wakulima ili kupunguza ukali wa maisha, wakati huo Serikali ikijipanga namna ya kukisaidia kiwanda hicho kiweze kuinuka.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda hicho, Bw. Jefferson Mofwi amesema amepokea maagizo hayo na watajitahidi kulipa stahiki hizo mapema iwezakanavyo kwani kiwanda kina Miradi mingine ya kuchakata mbao.
“Hivyo ndani ya kipindi cha miezi mitatu tutajitahidi kukamilisha, na hii yote ilichangiwa na kiwanda kukumbwa na changamoto za kiuzalishaji”. Amesema Mofwi.
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Ifwagi Matulizo Kanyika amemshukuru Naibu Waziri kwa kufika kiwandani na kusema Kuna maswali alikuwa anaulizwa na wananchi anashindwa kuyajibu na sasa yameshajibiwa.
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara yupo mkoani Iringa kwa ziara ya siku 2 lengo la ziara hiyo ni kutembelea baadhi ya viwanda vilivyopo mkoani humo kwa lengo la kuona, kukagua uzalishaji na kusikiliza changamoto na mapendekezo ya kuboresha zaidi.