Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu, Bw. Mohammed Kiande, akizungumza na Timu ya Wataalam ya kutoa Elimu ya Fedha, kutoka Wizara ya Fedha na Taasisi zake, walipofika Ofisini kwake kabla ya kuanza kutoa elimu ya fedha ikiwa ni mwendelezo wa zoezi la kutoa elimu hiyo kwa wananchi wa makundi mbalimbali katika Kata ya Nyigogo, Wilaya ya Magu, Mkoa wa Mwanza
Na Chedaiwe Msuya, WF, Mwanza
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu, mkoani Mwanza, Bw. Mohammed Kiande, amewataka wananchi kupanga matumizi yao vizuri, kuepuka madeni yasiyokuwa ya lazima, kujenga utajiri na kuongeza Uelewa wa Masuala ya kiuchumi.
Bw. Kiande alitoa rai hiyo wakati alipokutana na Timu ya Wataalamu kutoka Wizara ya Fedha, Taasisi za Serikali na Binafsi ambayo ipo mkoani Mwanza kwa ajili ya kutoa elimu ya fedha kwa makundi mbalimbali.
“Kupitia elimu hii, unaweza kuwekeza katika mipango ya muda mrefu kama vile akiba ya kustaafu na uwekezaji wa mali kupitia maarifa haya yatasaidia kutambua fursa na kuepukana na uwekezaji wa hatari au udanganyifu”, alisema Bw. Kiande.
Aliongeza kuwa Wananchi wajifunze jinsi ya kutengeneza bajeti inayolingana na kipato chao na kuweka akiba kwa ajili ya dharura na kufanya uwekezaji katika hisa, ardhi pamoja na biashara.
Bw. Kiande alifafanua kuwa elimu ya fedha siyo tu ni muhimu kwa kuimarisha maisha ya kifedha, bali pia kwa kujenga jamii yenye uelewa bora wa masuala ya kiuchumi.
“Ikiwa kila mtu atachukua jukumu la kujifunza na kutumia maarifa hayo, tunaweza kupunguza changamoto za kifedha na kuimarisha uchumi wetu kwa ujumla”. Alisema Bw. Kiande.
Nae mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Bw. Mussa Gwandake, alitoa pongezi kwa Wizara ya Fedha kwa kuwaletea elimu ya fedha katika mkoa wa Mwanza kwani elimu hiyo itawasaidia katika kukuza uchumi wao.
“Mafunzo haya yametufunza mbinu bora za usimamizi wa rasilimali, uwekaji akiba, na kuepuka madeni yasiyo ya lazima, tunathamini juhudi zenu katika kuinua uelewa wa wananchi kuhusu masuala ya kifedha. Asanteni kwa kujali ustawi wetu wa kiuchumi” alisema Bw. Gwandake.
Kwa upande wake Afisa Usimamizi wa Fedha, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha Bw. Salim Khalfan Kimaro, alisema kuwa kupitia elimu ya fedha ni nguzo muhimu ya maendeleo ya kiuchumi kwa jamii kwa kuwa na mwongozo wa kutosha kuhusu kuchukua mikopo yenye tija na kupaswa kufanya tathmini kabla ya kukopa ili kuepuka madeni yasiyo na faida kwao.
“Ni muhimu kuwaelimisha kuhusu hatari za kukopa kutoka kwa taasisi zisizosajiliwa rasmi na kupaswa kuchagua taasisi za kifedha zilizoidhinishwa na Benki Kuu ya Tanzania, ( BoT) ili kuhakikisha usalama wa fedha”, alisema Bw. Kimario
Nae Mratibu wa Huduma Ndogo za Fedha wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu, Bi Lilian Michael, aliishukuru Wizara ya Fedha kwa kuwapatia elimu wananchi wa Mkoa wa Mwanza kwani itasaidia kuwafumbua macho wananchi na kuepukana na migogoro ya familia inayojitokeza.
“Kabla ya kukopa, ni vyema familia ijadili madhumuni ya mkopo, masharti yake na athari zake kwa kila mwanakaya kwani itasaidia kupima iwapo kuna njia mbadala za kupata fedha badala ya kukopa’’, alisema Bi. Lilian


Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu, Bw. Mohammed Kiande, akizungumza na Timu ya Wataalam ya kutoa Elimu ya Fedha, kutoka Wizara ya Fedha na Taasisi zake, walipofika Ofisini kwake kabla ya kuanza kutoa elimu ya fedha ikiwa ni mwendelezo wa zoezi la kutoa elimu hiyo kwa wananchi wa makundi mbalimbali katika Kata ya Nyigogo, Wilaya ya Magu, Mkoa wa Mwanza.

Afisa Usimamizi wa Fedha Mwandamizi kutoka, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bw. Salim Khalfan Kimaro, akitoa mada kuhusu masuala ya fedha na umuhimu wa kusajili vikundi vya kutoa Huduma Ndogo za Fedha na vile vya kijamii kwa wananchi wa Kata ya Nyigogo, kwenye program maalum ya elimu ya fedha iliyotolewa kwa wananchi katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu Kata ya Nyigogo, Mkoa wa Mwanza.


Baadhi ya wajasiriamali na wananchi kutoka Kata ya Shishani, Kisesa na Nyanguge Wilaya ya Magu, mkoani Mwanza, wakiwa katika Ukumbi wa Halmashauri ya Magu pamoja na Timu ya Wataalamu wa Elimu ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha na Taasisi zake Wilayani humo, wakichangia mada mbalimbali kuhusu elimu ya fedha waliyoipata kupitia njia ya filamu yenye maudhui kuhusu matumizi sahihi ya fedha, umuhimu wa kupanga bajeti na kuitekeleza, umuhimu wa kusajili vikundi vya huduma ndogo za fedha , utunzaji wa fedha binafsi, umuhimu wa kushirikisha familia na watu wa karibu kwenye masuala ya fedha na uwekezaji, umuhimu wa kukata bima ya biashara na mali nyingine.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-WF, Mwanza)