Featured Kitaifa

IAA YAJIDHATITI KUWEKEZA KWENYE MADARASA MTANDAO MWAKA 2025/2026

Written by mzalendoeditor

 

Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Prof. Eliamani Sedoyeka amesema IAA katika mwaka wa fedha 2025/2026 imejipanga kuwekeza zaidi ya shilingi bilioni nne katika teknolojia za kufundishia na kujifunzia ikiwa ni pamoja na madarasa mtandao (smart classes).

Prof. Sedoyeka ameyasema hayo wakati wa Ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) leo tarehe 21 Machi 2025 katika Kampasi ya Arusha, ziara iliyolenga kukagua miradi mbalimbali ya ujenzi wa miundombinu ya Chuo inayoendelea. 

Amesema lengo la uwekezaji ni kuboresha mazingira ya kujifunzia kuendana na kasi ya maendeleo ya TEHAMA katika kuwafikia wanafunzi wengi kwa wakati mmoja, ” kupitia ‘smart classes’ mwalimu ataweza kufundisha akiwa katika Kampasi mojawapo Kati ya Arusha, Dar es Salaam, Babati, Dodoma na Songea na wanafunzi wakajifunza popote walipo”.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Mhe. Japhet Hasunga amesema uwekezaji utasaidia IAA kuwa  Chuo mfano katika kutoa Elimu Kitaifa na kimataifa. 

Ameongeza kuwa kupitia madarasa mtandao hata wanafunzi kutoka nje ya nchi wataweza kusoma na yatasaidia wanafunzi kupata Elimu katika ubora unaofanana kwa kuwa Mwalimu mmoja kutoka katika Kampasi moja ataweza kufundisha watu wengi kutoka maeneo tofauti kwa wakati mmoja.

Kwa upande wake mjumbe wa Kamati ya PAC, Mhe. Cendester Sichalwe ambaye ni mhitimu wa IAA, ametoa wito kwa wazazi na Watanzania wote kukiamini Chuo cha Uhasibu Arusha na kukifanya kuwa chaguo lao la kwanza kwa kuwa watakaposoma au kuleta watoto wao watapata Elimu Bora na inayoishi.

“Mimi nimesoma IAA kwa zaidi ya miaka saba naifahamu IAA, natoa wito kwa wanaohitaji kusoma chuo kuja IAA; Chuo hiki kina vielelezo vyote vya kumfanya mhitimu kukabili soko la ajira Kitaifa na Kimataifa; mimi nilivyomaliza Chuo ajira yangu ya kwanza ni kwenye mashirika ya Kimataifa na nimekuwa nikifanya kazi huko pia kabla sijawa mbunge”, amesema Sichalwe.

Aidha, Mhe. Sichalwe ameongeza kuwa uboreshaji wa miundombinu inayoendelea kufanyika IAA kupitia mapato ya ndani na fedha kutoka serikali Kuu umelenga kuwafanya Watanzania kupata mazingira rafiki yatakayowawezsha kupata Elimu Bora itakayowawezesha kutoa mchango katika maendeleo ya Jamii na Taifa kwa ujumla.

 

 

About the author

mzalendoeditor