Featured Kitaifa

BALOZI NCHIMBI ACHANGISHA SH. 950 MILIONI KWA MATIBABU YA WAGONJWA WA MGUU KIFUNDO

Written by mzalendoeditor

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, amefanikisha uchangishaji wa shilingi milioni 950 kwa ajili ya matibabu ya watoto wapatao 400 wanaougua ugonjwa wa mguu kifundo.

Kiasi hicho cha fedha kimepatikana kupitia ahadi za wadau mbalimbali walioshiriki hafla ya futari maalum kwa harambee hiyo, iliyofanyika Machi 14, 2025, katika Ukumbi wa Super Dome, Dar es Salaam. Harambee hiyo ililenga kukusanya shilingi milioni 600 kwa ajili ya matibabu hayo.

Akifungua hafla hiyo kama mgeni rasmi, Balozi Nchimbi alisema tukio hilo ni sehemu ya kumuunga mkono Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ameleta mafanikio makubwa katika sekta ya afya.

“Siku chache zilizopita, Rais Dkt. Samia alitangazwa mshindi wa tuzo ya kimataifa kwa juhudi zake za kupunguza vifo vya mama wajawazito na watoto, na kuwa Rais wa kwanza barani Afrika kupata nishani hiyo,” alisema Balozi Nchimbi.

“Shughuli yetu ya leo ni ishara ya kuunga mkono kazi kubwa anayoifanya kwa taifa letu, ambayo imetambuliwa kimataifa,” aliongeza.

Aidha, Balozi Nchimbi alifichua kuwa baada ya kumtaarifu Rais Dkt. Samia kuhusu harambee hiyo—iliyodhaminiwa na Taasisi ya GSM kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Klabu ya Yanga, na Hospitali ya CCBRT—Rais alielekeza CCM ichangie shilingi milioni 50 kwa ajili ya kusaidia matibabu hayo.

About the author

mzalendoeditor