Featured Kitaifa

WATUMISHI NELSON MANDELA WAJENGEWA UWEZO ELIMU KUHUSU UKATILI WA KIJINSIA

Written by mzalendoeditor

 

Naibu Makamu Mkuu wa Taasisi Mipango, Fedha na Utawala,Prof.Suzana Augustino akiongea na watumishi wanaume wakati wa ufunguzi wa warsha ya wanaume Machi 14,2025 Jijini Arusha

…….

Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) imendesha warsha ya siku mbili ya kuwajengea uwezo watumishi wanaume, ikiwa ni kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuondokana na ukatili wa kijinsia na kuelimisha kuhusu umuhimu wa elimu jumuishi na afya bora ya akili katika maeneo ya kazi na jamii kwa ujumla.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Machi 14, 2025 jijini Arusha, Naibu Makamu Mkuu wa Taasisi Mipango, Fedha na Utawala Prof. Suzana Augustino kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Taasisi ameeleza kuwa, warsha hiyo imefadhilwa na Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET PROJECT) ambao una kipengele cha kuwajengea uwezo watumishi

“Naamini baada ya hizi siku mbili watumishi wetu wa kiume watakuwa na uelewa mpana wa namna ya kushirikiana na watu wenye ulemavu na changamoto mbalimbali, kuimarisha mashirikiano mazuri kazini na uelewa wa jinsi ya kuishi baina ya wanawake na wanaume kazini” alisema Prof. Suzana.

Alieleza kuwa, warsha hiyo italeta matokeo chanya kwa watumishi wote wa NM-AIST wanaume na wanawake kuongea lugha moja , kwa kuwa wanawake walishapatiwa mafunzo hayo hivyo kutoa huduma bora kwa wateja.

Naye Dkt. Rehema Horera mtoa mada katika eneo la ukatili wa kijinsia na unyanyasaji wa kingono kutoka Wizara ya Elimu , Sayansi na Teknolojia ameipongeza taasisi ya NM-AIST kwa kuona umuhimu wa kutoa mafunzo ya ndani kwa makundi tofauti tofauti kwa kuzingatia kuwa, wanaume ni nguzo muhimu katika kusimamia maadili , kuzuia ukatili wa kijinsia na kingono ndani ya taasisi na jamii kwa ujumla.

“Warsha kama hizi zinatusaidia kukumbushana kwa pamoja umuhimu wa kuendelea kusimamia maadili na kudhibiti vitendo vya ukatili wa kijinsia na unyanyasaji wa kingono katika taasisi, na maeneo tunayotoka ili kuweza kufanya shughuli zetu kwa ufanisi” alisema Dkt. Rehema

Naye mmoja wa washiriki wa warsha hiyo, Prof. Revocatus Machunda alieleza kuwa, kupitia warsha hiyo, imewajenga katika kuhakikisha wanalinda ustawi wa afya ya akili, kusimamia haki ya usawa kwa watu wote ili kutoathiri utendaji kazi katika maeneo ya kazi na kuwa mabalozi wema kwa jamii zinazowazunguka katika kuwaelimisha masuala hayo.

Kwa Upande wake Bw. Denis Nandi Afisa Masoko Mwandamizi ameeleza kuwa, warsha hiyo ni chachu kwa watumshi kuimarisha ushirikiano mzuri katika eneo la kazi na jamii kwa ujumla hivyo kuleta tija katika utendaji.

Warsha hiyo ya siku mbili imewakutanisha watumishi wanaume zaidi ya 120 kutoka ngazi ya uongozi, wahadhiri, utawala na watendaji wa kiufundi ambapo wameweza kujengewa uwezo katika masuala ya afya ya akili, ukatili wa kijinsia, unyanyasaji wa kingono, elimu jumuishi pamoja na kukabiliana na msongo wa mawazo.

Naibu Makamu Mkuu wa Taasisi Mipango, Fedha na Utawala,Prof.Suzana Augustino akiongea na watumishi wanaume wakati wa ufunguzi wa warsha ya wanaume Machi 14,2025 Jijini Arusha.

 Mwezeshaji na Mtoa Mada kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia,Dkt.Rehema Horera, akiwasilisha mada kuhusu Ukatili wa Kijinsia na Unyanyasaji wa kingono kwa watumishi wanaume kutoka Taasisi ya Nelson Mandela Machi 14,2025 jijini Arusha.

Dkt. Staricko Meshack kutoka Chuo cha Mipango akiwasilisha mada ya Jinsia na Dawati la Jinsia, wakati wa warsha ya wanaume wa Taasisi ya NM-AIST Machi 14,2025 jijini Arusha.

Prof. Ernest Mbega Amidi wa Shule Kuu ya LiSBE akimuwakilisha Naibu Makamu Mkuu wa Taasisi Taaluma, Utafiti na Ubunifu akiongea neno wakati wa warsha ya wanaume wa Taasisi ya NM-AIST Machi 14,2025 Jijini Arusha

Watumishi wanaume wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela wakifuatilia mada mbalimbali wakati wa warsha iliyoandaliwa kwa ajili ya wanaume wa Taasisi hiyo Machi 14,2025 Jijini Arusha.

BW.Emmanuel Lema Mhasibu kutoka Taasisi ya NM-AIST akichangia jambo wakati wa Warsha ya wanaume wa Taasisi hiyo iliyofanyika Machi 14,2025 Jijini Arusha.

About the author

mzalendoeditor