Featured Kitaifa

WANAWAKE BADO WANAKUMBANA NA UKATILI WA KIJINSIA – JAJI MWAIMU

Written by mzalendo

Na Gideon Gregory, Dodoma.

Katika kuelekea maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani Machi 8, Tume ya Haki za Binandamu na Utawala Bora (THBUB), imesema bado wanawake wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo vitendo vya ukatili wa kijinsia na uwezo mdogo wa kushiriki shughuli za kiuchumi na kisiasa.

Hayo yameelezwa leo Machi 7,2025 hapa Jijini Dodoma na Mwenyekiti wa tume hiyo Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu wakati aklizungumza na
waandishi wa habari kuelekea maadhimisho hayo ambayo kitaifa yatafanyika Jijini Arusha huku akitoa mapendekezo mbalimbali kwa Serikali.

“THBUB inatambua jitihada mbalimbali za Serikali na wadau wengine katika kuhakikisha wanawake wanapata haki zao na kuwawezesha kisiasa,kiuchumi na kijamii. Lakini pamoja na jitihada hizo wanakabiliwa na changamoto zikiwemo vitendo vya ukatili wa kijinsia na uwezo mdogo wa kushiriki shughuli za kiuchumi na kisiasa”.

Ambapo Jaji Mstaafu Mwaimu ametoa mapendekezo ma nne kwa Serikali na Wadau ikiwemo kuendelea kuwezesha wanawake kiuchumi na kisiasa ili kuleta usawa katika jamii, pia Serikali na Wadau wengine kuendelea kutoa elimu itakayo wasaidia wanawake kutambua haki zao na kuzidai zinapovunjwa.

“Kutokana na changamoto hizo THBUB inapendekeza kuwa Serikali iendelee kuwawezesha wanawake kiuchumi na kisiasa ili kuleta usawa katika jamii,Serikali na wadau wengine waendelee kutoa elimu itakayo wasaidia wanawake kutambua haki zao nankuzidai zinapovunjwa,Jamii kuendelea kuzingatia sheria,haki haki za binadamu na misingi ya utawala bora ili kuleta usawa na wanawake wenyewe kuendelea kujiamini na kutumia fursa zilizopo kujiwezesha kiuchumi na kisiasa”.

Aidha amesema kuwa kauli mbiu ya mwaka huu inatukumbusha kuhusu wajibu wa jamii kuona umuhimu wa ujumuishi wa wanawake na wasichana katika mipango yote ya maendeleo,kusimama kidete kuhakikisha wanapata haki zao na fursa sawa katika nyanja zote za Maendeleo.

Ameongeza kuwa kuwa kupitia Kaulimbiu hiyo jamii pia inapata fursa ya kujadili na kuandaa mikakati madhubuti itakayo saidia kutatua changamoto zinazowakabili wanawake, wasichana na makundi mengine yenye mahitaji maalum,zikiwemo zile zinazotokana na ukatili wa kijinsia ili kuleta usawa.

Umoja wa Mataifa uliridhia na kuanza kuadimisha rasmi siku ya Wanawake Duniani Machi 8 mwaka 1975 kwa lengo la kuikumbusha Dunia juu ya usawa wa kijinsia na Haki za Wanawake.

About the author

mzalendo