Na Imma Msumba : Arusha
Naibu mkuu wa Chuo Fedha, Mipango na Utawala Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Dkt. Grace Temba, amesema kuwa wanatambua mchango mkubwa wa viongozi, watumishi wanawake na wanafunzi wa kike katika maendeleo endelevu ya chuo hicho.
Akizungumza mara baada ya kutembelea banda la chuo hicho lililopo katika maonesho yanayoendelea katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid kuelekea siku ya Kimataifa ya wanawake Duniani ameeleza kuwa mafanikio ya chuo hicho yanatokana kwa kiasi kikubwa na mchango wa watumishi wanawake na kwamba chuo kitaendelea kuwawezesha wanawake katika nyanja mbalimbali ili kuwainua kiuchumi na kijamii.
“IAA tunaienzi Kauli mbiu ya maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya Wanawake mwaka huu kwa vitendo.Uongozi unatambua mchango wa wanawake katika Maendeleo ya Chuo; IAA tunaongozwa na Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi, Dkt. Mwamini Tulli (mwanamke), Wasaidizi wa wawili wa Mkuu wa Chuo upande wa Utawala na Taaluma ni wanawake, tuna viongozi wanawake pia kwenye Idara mbalimbali na wanafanya kazi nzuri”, amesema Dkt. Temba.
Amebainisha kuwa chuo hicho kinaendelea kuwawezesha wanafunzi, hususani wa kike, kwa kuwapa mafunzo ya ujasiriamali na ubunifu wa biashara kupitia kiatamizi cha IAA Business Startup Centre (IBSUC), ili waweze kujiajiri na kuajiri wengine baada ya kuhitimu masomo yao.
Aidha, amewahimiza wanafunzi wa kike kutoogopa kusoma masomo ya sayansi na kutumia fursa zinazotolewa na chuo ili kuwawezesha kielimu na kiuchumi.
Hata hivyo kwa upande wake msimamizi wa kiatamizi cha IAA Business Startup Centre IBSUC, Sarah Mwaisumo amesema wamefanikiwa kuwa na wanafunzi wajasiriamali waliofanikiwa kuanzisha kampuni zaidi ya 80 ambazo zinaendelea kufanya vizuri katika sekta mbalimbali za biashara, TEHAMA ambapo kupitia kiatamizi wanafunzi wanapata mafunzo ya ujasiriamali, usimamizi wa biashara, na mbinu za ubunifu ambazo zinawasaidia kuanzisha na kuendesha kampuni zao kwa ufanisi.
Rejoice Daniel ni Mwanafunzi wa diploma mwaka wa kwanza na mjasiriamali, ambaye yupo chini kiatamizi cha IBSUC ambapo ameshukuru chuo kwa kuwawezesha wanafunzi wa kike kupata nafasi ya mafunzo hayo kwa vitendo kupitia programu hiyo, na kwamba zinawasaidia wasichana kujitegemea kiuchumi na kuchangia maendeleo ya jamii.
Siku ya kimataifa ya wanawake kwa mwaka huu inaongozwa na kaulimbiu isemayo ” Wanawake na Wasichana 2025: Tuimarishe Haki, Usawa na Uwezeshaji”