Na Mwandishi Wetu
Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deus Sangu amewataka Wataalam wa Kumbukumbu na Nyaraka (TRAMPA) kuhakikisha wanatunza siri wanazoziona na kusoma kwenye kumbukumbu na nyaraka mbalimbali kwa ustawi na usalama wa taifa kwa jumla.
Ametoa rai hiyo leo tarehe 6 Machi, 2025 wakati wa kufunga Kikao Kazi na Mafunzo Maalum kwa Wataalam wa Kumbukumbu na Nyaraka (TRAMPA) kinachofanyika jijini Mbeya.
“Kiapo cha utunzaji siri na uadilifu mlichokipata ni sehemu ya misingi ya utunzaji kumbukumbu na nyaraka kwa manufaa mapana ya Taifa, pasipo kutunza siri na kuzingatia maadili mengine yaliyowekwa kisheria itakuwa ni vigumu kupanga na kutekeleza mipango mikakati ya nchi” amesisitiza Mhe. Sangu.
Aidha, Mhe. Sangu amewataka wanataluma hao kuendelea kupigania ustawi wa taaluma yenu ambayo ni kiungo muhimu cha uendeshaji na utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya taifa, na msichoke kupaza sauti juu ya wanataaluma wengine wanaotaka kuharibu taswira nzuri ya kada hii.
Vilevile, amesisitiza Wataalam hao kuendelea kuchapa kazi kwa kuzingatia matakwa ya Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo ambayo imekuwa ikitolewa na Mamlaka husika kwa nyakati tofauti.
Ametoa wito kwa Waajiri wote katika taasisi za umma kuhakikisha wanatumia mfumo wa kielektroni wa utunzaji kumbukumbu na nyaraka (e-office) ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi, tija na kwenda sambamba na mabadiliko ya ukuaji wa sayansi na teknolojia.
Awali, Mwenyekiti wa TRAMPA Bi. Devotha Mrope ameiushukuru Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa kuendelea kuisimamia na kuilea TRAMPA ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Pia, amesema TRAMPA itaenelea kuratibu mafunzo na kikao kazi hicho kila mwaka kwa lengo la kuongeza ujuzi na ari ya wanachama kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Naye, Mkurugenzi, Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini-TRAMPA Bw. Firimin Msiangi amesema jengo linalotarajiwa kujengwa jijini Dodoma litakuwa ni kitenge uchumi kimubwa cha TRAMPA na hivyo kuwa na uwezo wa kujiendesha.
TRAMPA ilianzishwa 2013 na ina Wanachama 7500 kutoka sekta ya umma na binafsi kwa Tanzania bara na Visiwani. Kikao Kazi na Mafunzo hayo yaliyoanza tarehe 2-6 Machi, 2025 Jijini Mbeya yanahusisha washiriki zaidi ya 1, 500 na kuongozwa na kaulimbiu isemayo “Misingi Bora ya Utunzaji wa Kumbukumbu na Nyaraka ni Nguzo Muhimu Kitaaluma”.