OR TAMISEMI
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais – TAMISEMI anayeshughulikia Miundombinu Mhandisi Rogatus Mativila, amewataka wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa ofisi hiyo kufanya kazi kwa bidii ili kuendana na kasi ya Serikali.
Akizungumza leo Machi 4, 2025, jijini Dodoma wakati wa kikao cha baraza hilo, Mhandisi Mativila, amesema baraza lina nafasi muhimu katika kuongeza ushiriki wa wafanyakazi kwenye uendeshaji wa taasisi na kuboresha utendaji kazi.
“Tija na maslahi lazima viwe na uwiano ili kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi,” amesema.
Naye, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Emma Lyimo, amesisitiza umuhimu wa vikao hivyo, akiwataka wakuu wa idara na vitengo kushiriki kikamilifu ili kusaidia kutatua changamoto za watumishi.
Kikao hicho cha siku mbili kinatoa fursa kwa watumishi kujadili masuala mbalimbali na kujengewa uwezo wa utendaji kazi.