Featured Kitaifa

BODI YA TBS YAFANYA ZIARA YA UKAGUZI WA MRADI WA UJENZI WA VIWANGO HOUSE JIJINI DODOMA

Written by mzalendoeditor

Bodi ya wakurugenzi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS)imetoa maagizo kwa mkandarasi anayejenga jengo la Shirika hilo kuhakikisha ujenzi unakamilika.

Hayo yamebainishwa hii leo tarehe 27/2/2025 na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TBS, Prof.Othman Chande Othman wakati walipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa jengo hilo mkoani Dodoma.

Prof.Othman amesema kuwa ujenzi unaendelea vizuri kwani mpaka sasa jengo hilo limefikia 72% huku mategemeo yao ndani ya mwaka huu 2025 ujenzi huo utakamilika na maabara zitaanza kufanya kazi rasmi jijini Dodoma.

Amebainisha kuwa changamoto iliyokuwepo hapo awali ni upatikanaji wa vifaa kwani mradi huo unahusisha ujenzi wa maabara ambazo zinahitaji vifaa maalum na vya kisasa na vyote vinatoka nje ya nchi.

“Sisi tunashughuli za maabara kwa hivyo maabara inahitaji vifaa maalumu ambavyo vyote tunaagiza nje na mchakato ulishaanza na tunasubiria vifaa hivyo kuingia nchini kwa ajili ya kufungwa ili kukamlilisha maabara hizo”amesema Prof.Othman.

Msimamizi wa mradi kwa upande wa Mkandarasi Mshauri Mhandisi.Dkt. Johnson Malisa amesema kazi za awali zimekamilika kwa zaidi ya 90% na kazi iliyobakia ni ukamilishaji (finishing).

Mhandisi Malisa amesema TBS tayari imezifanyia kazi changamoto zote ambapo kwa sasa vifaa vimekwisha agizwa hivyo mategemeo yao ni nguvu ya kazi itaongezeka na kukamilisha mradi kwa wakati.
Kukamilika kwa jengo hilo kutakua na tija kwani kutasogeza huduma karibu na wadau wa kanda ya kati na mikoa ya karibu.

About the author

mzalendoeditor