Featured Kitaifa

TEA YATENGA BILIONI TATU KUBORESHA  MIUNDOMBINU NA VIFAA VYA MAFUNZO YA AMALI KWA SHULE 20 NCHINI

Written by mzalendoeditor

 

Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) Dkt. Erasmus Kipesha, wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari leo Februari 25,2025 jijini Dodoma kuhusu mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita katika sekta ya Elimu nchini.

Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) Dkt. Erasmus Kipesha, wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari leo Februari 25,2025 jijini Dodoma kuhusu mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita katika sekta ya Elimu nchini.

 Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari-MAELEZO,Bi.Zamaradi Kawawa,akitoa shukrani kwa waandishi wa habari mara baada ya Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) Dkt. Erasmus Kipesha,kutoa taarifa kuhusu mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita katika sekta ya Elimu nchini.

Waandishi wa habari wakimsikiliza Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) Dkt. Erasmus Kipesha , wakati akitoa taarifa  kuhusu mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita katika sekta ya Elimu nchini.

Na.Alex Sonna-DODOMA
KATIKA kutekeleza Sera mpya  ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 toleo la Mwaka 2023, Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) imetenga shilingi bilioni 3 kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu na vifaa mbalimbali vya mafunzo ya amali kwa shule 20 nchini.
Hayo yamebainishwa leo Februari 25,2025 jijini Dodoma na Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) Dkt. Erasmus Kipesha,wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita katika sekta ya Elimu nchini.
Dkt.Kipesha amesema kuwa wajibu wao ni kuhakikisha wanaunga mkono utekelezaji wa Sera hiyo ya Elimu kwa kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia kwa maana ya ujenzi wa vyumba vya madarasa, maabara za Sayansi, nyumba za walimu na vifaa mbalimbali vya mafunzo ya amali kama michezo, ushoni, mapishi, kilimo, sanaa na TEHAMA
“Kwa sasa tumetenga shilingi bilioni 3 kwa ajili ya miundombinu ya amali kwenye shule 20 hapa nchini pamoja na vifaa mbalimbali vya amali ambavyo vitakuwa mkombozi na kuchochea kukua kwa elimu bora na ya kiwango”amesema Dkt.Kipesha
Aidha amesema kuwa watahakikisha wanaimarisha miundombinu ya elimu kote nchini  kuunga mkono utekelezaji wa sera ya elimu kwa kuwa na miundombinu na vifaa vya mafunzo ya amali.
“Jukumu letu kubwa ni kuimarisha na kuboresha miundombinu ya kujifunzia na kufundishia kwa kujenga vyumba vya madarasa, matundu ya vyoo, nyumba za walimu, maabara, mabweni pamoja na kuweka vifaa mbalimbali vya elimu vya mafunzo ya amali.
Hata hivyo ameeleza kuwa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuwakomboa vijana wa Kitanzania kwa kuboresha sera ya elimu na mafunzo ambapo vijana wengi wataweza kujiajiri au kuajiriwa mahali popote nchini kulingana na ujuzi watakaoupata mashuleni.

Aidha Dkt.Kipesha,ametoa wito kwa wadau mbalimbali nchini kuendelea kuiunga mkono Serikali kwa kuchangia sekta ya elimu kupitia Mfuko wa Elimu wa Taifa.

“Kuna faida ya kuchangia maendeleo ya elimu kupitia Mfuko wa Elimu wa Taifa ila hatuwalazimishi kupitia TEA ila kwa namna yeyote ambavyo mdau atachangia lengo ni kuendeleza sekta ya elimu,” ameeleza Dkt.Kipesha

About the author

mzalendoeditor