Na MwandishiWetu, Dodoma.
Wazazi na walezi wenye watoto wenye matatizo ya moyo wameombwa kuwaleta kwenye kambi ya matibabu ya moyo ya ushirikiano wa mabingwa wa Benjamin Mkapa Hospital na Kuwait kwa watoto iliyoanza tarehe 21 mpaka 28 Februari hapo BMH
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa BMH, Prof Abel Makubi, wakati akiongea na waandishi wa habari kuhusu kambi ya pamoja ya matibabu ya moyo kwa watoto inayotekelezwa na BMH na madaktari bingwa wa moyo kutoka Shirika la Children Heart Association la Kuwait.
“Kwahiyo, nawaomba wazazi au walezi wenye watoto wenye matatizo ya moyo watumie fursa hii kuwaleta watoto hapa BMH wafanyiwe uchunguzi ili wakikutwa na tatizo la moyo wafanyiwe upasuaji,” amesema Mkurugenzi Mtendaji wa BMH.
Timu ya wataalamu wa magonjwa ya moyo kumi na sita (16) kutoka Shirika la Children Heart Association la Kuwait wanafanya kambi kwa pamoja ya matatizo ya moyo kwa watoto na madaktari bingwa wa moyo wa Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) ya jijini Dodoma.
Prof Makubi ametaja dalili za matatizo ya moyo kwa watoto kuwa ni kupumua kwa shida, kikohozi cha mara kwa mara, mtoto kushindwa kunyonya na kutokwa na jasho jingi na kutoongezeka uzito.
“Dalili nyingine kwa mtoto mwenye matatizo ya moyo ni kupata fatigue (kuchoka sana) na kushindwa kuhimili mazoezi,” amesema Prof Makubi.
Prof Makubi ametumia fursa hiyo kuwashukuru timu ya wataalamu wa moyo kutoka Kuwait kwa ushirikiano na BMH na ushirikiano huo ulianza mwaka 2023 na mwaka 2024 BMH ikasaini makubaliano na Shirika hilo la Children Heart Association.
Kwa upande wake, kiongozi wa msafara wa timu ya wataalamu kutoka Kuwait, Prof. Faisal Al-Saidei, amesema lengo la wao kushirikiana na BMH ni kutoa matibabu ya moyo kwa watoto waliozaliwa na matatizo ya moyo.
“Pamoja na kufanya kambi ya pamoja ya matibabu ya moyo kwa watoto pia tunajenga programu ya ushirikiano na Hospitali ya Benjamin Mkapa,” amesema Prof Al-Saidei.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Tiba wa BMH, Dkt. Kessy Shija, magonjwa ya moyo kwa watoto yanaweza kuchangiwa na NCDs, na maambukizi kwa wazazi au mtoto, kuzaliwa kabla ya wakati na kurithi .