Na Mwandishi Wetu Mbozi, Songwe
Walanguzi wa mazao ya wakulima wa kahawa, mahindi, mbogamboga na karanga wameondoka baada ya kukamilika kwa ujenzi wa barabara ya Ilolo-Ndolezi yenye urefu wa Km 11.01 kwa kiwango cha lami katika halmashauri ya wilaya ya Mbozi mkoani Songwe.
Wakiongea kwa nyakati tofauti baadhi ya wakazi wa kitongoji cha Isiniza kijiji cha Mbimba wamesema kuwa barabara hiyo imewarahisishia kusafirisha mazao yao kutoka mashambani hadi kwenye masoko, hivyo kuwaongezea kipato.
Bi. Salome Nzunda amesema wanaishukuru serikali kwa kuwajengea barabara hiyo ambapo zamani ilikuwa na changamoto sana kwani barabara haikuwa inapitika.
“Zamani tulikuwa tunapita barabara ya kutoka Vwawa kwenda Ndolezi, ilikuwa na changamoto sana hata mtu akiumwa kwenda hospitali ya wilaya ilikuwa kazi, barabara ilikuwa haipitiki hata vifo vya wajawazito na watoto vilikuwepo sana”
“Tulikuwa tunashindwa kupita kwenye barabara hii, ilikuwa tope haswa na tulikuwa tukitumia hadi saa mbili kwenda mjini, lakini sasa hivi tunatumia dakika 15 kufika mjini, tunaishukuru serikali wametutengenezea barabara hii tunaweza kufika hospitali ya wilaya hata ya mkoa na vifo sasa hivi vimepungua”, aliongeza.
Vile vile amesema kwamba, barabara hiyo imeondoa pia walanguzi wa mazao yao ambapo awali walanguzi hao walikuwa wakipita kwenye nyumba zao na kununua mazao kwa bei ya chini, lakini hivi sasa wanasafirisha wao wenyewe kwenda kuuza kwenye soko kuu la Vwawa mjini, hivyo kuwaongezea kipato na kuweza kuimarisha maisha yao kwa kujenga nyumba za bati tofauti na zamani walikuwa na nyumba za nyasi.
Naye, Bw. Heckson Mwambalo mkazi wa kijiji cha Mbimba amesema kuwa, wananchi wamefurahi sana kwani imewasaidia kusafirisha mazao yao kwa urahisi.
“Tunaishukuru serikali kwa kutuona na kutujengea barabara hii kwani njia hii kutoka Vwawa, Idiwili kwenda Ndolezi haikuwa inapitika, mvua ikinyesha hatukuwa tunafanya chochote tulikuwa tukisubiri jua litoke ndiyo twende kuchukua mazao kwa kweli wananchi wote tumefurahi.
Kaimu Meneja wa TARURA mkoa wa Songwe, Mhandisi Lugano Mwambingu amesema barabara ya Ilolo-Ndolezi imejengwa kupitia mradi wa Agri-Connect kwa thamani ya Shilingi Bilioni 6.46 na hadi sasa umekamilika kwa 100%.
Amesema barabara hiyo imejengwa kwa kiwango cha lami pia wamejenga safu za boksi kalavati (3), safu za zege 35 kuweka alama za barabarani 50, mfereji wa maji ya mvua Km 6.456 pamoja na kuweka taa za barabarani 40.
Aidha, Mhandisi Mwambingu ameongeza kusema kwamba barabara hiyo imesaidia kuongeza uzalishaji wa mazao ya biashara pamoja na mpango wa kurahisisha mawasiliano kwa wananchi wanaoishi katika Kata za Iyula, Idiwili na Mlangali.
“Barabara hii imekuwa na muhimu sana kwa wakulima wa vijiji hivi kwani imefungua fursa za kiuchumi katika bonde hilo kwani kila zao linakubali na kuinua kipato cha mwananchi mmoja mmoja.
Ameongeza kusema kwamba barabara hiyo imewarahisishia wakulima kupeleka kahawa yao kiwandani pia mazao mengine kwenye masoko pamoja na kupeleka katika maghala ya kuhifadhia mazao yaliyopo mjini.
Mkoa wa Songwe unahudumia mtandao wa barabara wa Km. 3,341.628 ambapo barabara za lami Km.36.38, changarawe Km. 1155.718, udongo Km. 2,149.53, madaraja 212 pamoja na makalavati 1,971.