JUMLA ya watu 47 wameripotiwa kufariki nchini Afghanistan katika majimbo ya Khost na Kunar yanayopatikana mashariki mwa nchi hiyo na hiyo ni baada ya shambulio la anga lililotekelezwa na majeshi ya Pakstan.
Mkurugenzi wa Taarifa na Utamaduni wa Jimbo la Khost Shabir Ahmad Osmani amenukuliwa akiliambia Shirika la Habari la AFP kuwa:
“Raia 41 ambao wengi ni wanawake na watoto wamefariki dunia na wengine 22 wamejeruhiwa vibaya katika shambulio la anga lililotekelezwa na majeshi ya Pakistan karibu na Durand kwenye jimbo la Khost.
Naye Kiongozi wa Kunar alithibitisha kifo cha raia wengine sita katika jimbo lake ambapo picha kupitia Chombo kikubwa cha habari nchini humo TOLO zilionesha miili ya watoto wakiwa wamefariki, na ni chombo hichohicho ambacho kilionesha maelfu ya wakazi wa Khost wakipinga na kuikejeli Pakistan.
Majeshi ya Pakistan hayajatoa tamko lolote hadi sasa kuhusiana na tukio hilo japo siku ya Jumapili Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo akiwa Islamabad alielekeza viongozi wa Taliban huko Kabul kuhakikisha wanachukua hatua kali dhidi ya majeshi yanayoishambulia Pakistan kutokea katika ardhi ya Afghanstan.
“Magaidi wanatumia ardhi ya Afghanistan kwa uhuru kabisa kutekeleza mashambulizi dhidi ya Pakistan.”Alisema Shah Mahmood Qureshi Waziri wa mambo ya nje wa Pakistan.
Mgogoro wa mipaka kati ya Pakistan na Afghanistan imekua tangu Taliban walipochukua utawala wa nchi mwaka jana, huku Islamabad ikilaumu kuwa wapiganaji wanatekeleza mashambulizi kutokea katika ardhi ya Afghanistan.
Kwa upande mwingine hadi sasa duru za kisiasa zinadai kuwa bado haijawa wazi kama aziri Mkuu mpya wa sasa wa Pakistan Shebaz Sharif anaweza kuunga mkono uhusiano wa Afghanstan na Taliban kama ilivyokuwa kwa mtangulizi wake Imran Khan.