Featured Kitaifa

TAMISEMI YAWEKA WAZI VIWANGO VIPYA UJENZI WA MADARASA NA ZAHANATI

Written by mzalendo

OR-TAMISEMI

Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imefanya mapitio ya bajeti kwa kuzingatia muundo wa kanda na gharama za maisha ili kuhakikisha fedha zinazotengwa kwa miradi ya ujenzi zinatosheleza kukamilisha miundombinu muhimu.

Hivyo, kuanzia bajeti ya mwaka 2024/25, madarasa yatagharimu kati ya Sh.Milioni 22 hadi 25, huku ujenzi wa zahanati ukigharimu kati ya Sh.Milioni 284 hadi 358.

Naibu Waziri wa TAMISEMI, Mhe. Zainab Katimba, ameliambia Bunge leo Februari 13, 2025 alipokuwa akichangia taarifa ya mwaka ya utekelezaji wa majukumu ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC).

Amesema hatua hiyo imetokana na serikali kubaini tofauti kubwa ya gharama za vifaa vya ujenzi kati ya kanda mbalimbali, hali iliyokuwa ikikwamisha utekelezaji wa miradi muhimu kama shule, zahanati na majengo ya utawala.

“Tumefanya maboresho ya bajeti ili kuhakikisha miradi inakamilika kwa viwango sahihi. Kuanzia bajeti ya mwaka 2024/2025, madarasa yatagharimu kati ya shilingi milioni 22 hadi 25, huku ujenzi wa zahanati ukigharimu kati ya shilingi milioni 284 hadi 358,” amesema Mhe. Katimba.

Awali, Mwenyekiti wa Kamati ya LAAC, Mhe. Halima Mdee, amesisitiza kuwa kuanzia mwaka wa fedha 2025/2026, taasisi zote za umma zinazotoa huduma katika Serikali za Mitaa zinapaswa kushirikiana katika kuandaa miundombinu muhimu kama barabara, umeme, na maji kabla ya kuanza miradi yoyote ya ujenzi.

About the author

mzalendo