Featured Kitaifa

SAFARI ZA IRINGA ZAREJEA, TWIGA MILES KUTUMIKA KUKATA TIKETI

Written by mzalendoeditor

Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) inayo furaha kutangaza kurejesha safari za moja kwa moja kati ya Dar es Salaam na Iringa kuanzia Jumamosi, 22 Februari 2025.

Safari ya kwanza itaanza saa 3:00 asubuhi kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere na itachukua takribani dakika 60 kufika Uwanja wa Ndege wa Iringa. ATCL itaanza na safari tatu kwa wiki, Jumatatu, Jumatano na Ijumaa ikitumia ndege yake, DHC Q400 yenye uwezo wa kubeba abiria 6 katika Daraja la Biashara na 70 katika Daraja la Kawaida.

Nauli ya kwenda na kurudi ni TZS 199,200/= ikijumuisha mzigo wa hadi kilo 23, begi la mkononi lisilozidi kilo 7 pamoja na viburudisho ndani ya ndege bila malipo ya ziada. Wanachama wa Twiga Miles wataweza kulipia tiketi kwa kutumia pointi zao, huku wasafiri wapya wakipata zawadi ya pointi 3,000 wanapojiandikisha kupitia Air Tanzania Mobile App.

Mteja ataweza kukata tiketi yake kupitia tovuti: www.airtanzania.co.tz, Aplikesheni ya Simu ya Air Tanzania, Kituo cha Huduma kwa Wateja (+255748773900) au Ofisi za ATCL.

Kurejeshwa kwa safari hizi kunalenga kuboresha muunganiko wa usafiri kwa wafanyabiashara, watalii, wakazi wa Iringa na wasafirishaji wa mizigo hivyo kufungua fursa zaidi za kibiashara na maendeleo ya kiuchumi katika mkoa huo na maeneo jirani.

Imetolewa na:
Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano kwa Umma

About the author

mzalendoeditor