Featured Kitaifa

TAMISEMI YAKEMEA WANASHERIA WA HALMASHAURI WASIOWAJIBIKA

Written by mzalendo

OR-TAMISEMI

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mhe. Zainab Katimba, amewataka wakuu wa Idara na Vitengo vya Sheria katika Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha wanazingatia weledi, uadilifu, na uwajibikaji katika majukumu yao ili kuepusha uzembe unaoigharimu serikali.

Akizungumza Februari 12, 2025 kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mhe. Mohamed Mchengerwa, wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha siku mbili cha wakuu wa idara hizo jijini Dodoma, Mhe. Katimba amesema kuna uzembe wa hali ya juu katika usimamizi wa mashauri ya madai.

“Katika baadhi ya maeneo, mashauri ya madai yameendeshwa upande mmoja kwa zaidi ya miaka mitano na maamuzi kufikiwa dhidi ya serikali bila mwanasheria wa halmashauri husika kuhudhuria hata mara moja mahakamani,” amesema.

Ameongeza kuwa serikali haiwezi kuvumilia uzembe huu, hasa pale ambapo halmashauri hulazimika kulipa mabilioni ya shilingi baada ya kushindwa kesi kwa sababu ya kutohudhuria mahakamani au kusimamia vibaya mashauri.

Mhe. Katimba pia amebainisha changamoto katika usimamizi wa mikataba, ambapo baadhi ya mikataba hufikia ukomo bila mamlaka husika kuchukua hatua mapema za kuongeza muda wake, hali inayosababisha utekelezaji wa majukumu nje ya utaratibu wa kisheria.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Wakili Richard Odongo, amesema kikao kazi hicho kinalenga kujadili changamoto hizi na kuweka mikakati madhubuti ya kuongeza uwajibikaji na uadilifu katika sekta ya sheria ndani ya halmashauri.

About the author

mzalendo