Featured Kitaifa

WAJASIRIAMALI WADOGO KATA YA BOMAMBUZI NA NJORO WAPATA ELIMU YA FEDHA

Written by mzalendoeditor
Afisa Mkuu Mwanadamizi kutoka Wizara ya Fedha, Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Bw. Salim Kimaro, akitoa Elimu ya Fedha kwa Wajasiriamali Wadogo, waendesha BodaBoda na Vikundi vya Vikoba katika Kata ya Boma Mbuzi Wilaya ya Moshi Manispaa Mkoani Kilimanjaro.
Afisa Usimamizi Fedha Mwandamizi kutoka Wizara ya Fedha, Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha  Bw. Jackson Mshumba akigawa vipeperushi kuhusu Elimu ya Fedha kwa Mjasiriamali Mdogo, Bw. Godfrey Mwasha, wakati wa semina ya Elimu ya Fedha iliyofanyika katika Kata ya Boma Mbuzi Wilaya ya Moshi Manispaa Mkoani Kilimanjaro.
Mwanakikundi cha Vikoba, Bw. Omari Juma, akiuliza swali kwa mtoa mada (haonekani pichani) kuhusiana na uwekezaji wakati wa semina ya Elimu ya Fedha iliyofanyika katika Kata ya Boma Mbuzi Wilaya ya Moshi Manispaa Mkoani Kilimanjaro.
Afisa Mkuu Mwanadamizi kutoka Wizara ya Fedha, Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Bw. Salim Kimaro na Mchambuzi Fedha Mwandamizi kutoka Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) CPA Gladness Mollel wakitoa ufafanuzi wa maswali yalioulizwa na Wajasiriamali wadogo walioko kwenye Vikundi vya Vikoba Kata ya Njoro Wilaya ya Moshi Manispaa Mkoani Kilimanjaro.
Mchambuzi Fedha Mwandamizi kutoka Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) CPA Gladness Mollel akitoa mada kuhusiana na Uwekezaji kwenye hisa zilizoorodheshwa kwenye Soko la Hisa la Dar es salaam, Hati Fungani za Serikali na Kampuni pamoja na Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja kwa Wajasiriamali wadogo walioko kwenye Vikundi vya Vikoba Kata ya Njoro Wilaya ya Moshi Manispaa Mkoani Kilimanjaro.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Kilimanjaro)
Na Eva Ngowi, WF, KILIMANJARO
Serikali kupitia Wizara ya Fedha inaendelea kuwahamasisha wananchi Mkoani Kilimanjaro kushiriki kwa wingi katika semina kuhusu Elimu ya Fedha zinazoendelea kutolewa na Wizara kwa kushirikiana na Taasisi za Fedha nchini ili waweze kupata elimu ya matumizi sahihi ya huduma za fedha ikiwemo kuepuka kukopa kwa watoa huduma za fedha wasiosajiliwa kwa mujibu wa sheria.
Hayo yamesemwa na Afisa Mkuu Mwandamizi kutoka Wizara ya Fedha, Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Bw. Salim Kimaro wakati wa semina ya Wajasiriamali wadogo na Vikundi vya Vikoba iliyofanyika katika Kata ya Boma Mbuzi na Njoro Wilaya ya Moshi Manispaa Mkoa wa Kilimanjaro.
Bw. Kimaro aliwahimiza Wajasiriamali, Vyama vya Ushirika, Wanafunzi, Waalimu, Wafanyakazi, Vikundi vya Huduma Ndogo za Fedha na Wananchi wote kwa ujumla kuwa popote pale walipo waendelee kutufuatilia na kuhudhuria katika maeneo ambayo yatafanyika semina hizo ili waweze kujipatia Elimu ya Fedha kwa mustakabali wa Uchumi wao na Taifa kwa ujumla.  
Bw. Kimaro alisema malengo ya Elimu ya Fedha kwa Wananchi ni kuwajengea uwezo wa kufanya maamuzi sahihi ya kupata na kutumia huduma za fedha hapa nchini.
Alisema kuwa huduma hizo ni suala ambalo linapaswa kufahamika katika matumizi yake na upatikanaji wake ili kuwaepusha wananchi na changamoto mbalimbali zinazotokana na kutoelewa masuala mbalimbali ya Elimu ya Fedha na kujiepusha na mikopo kausha damu.
“Tumekuja Mkoa wa Kilimanjaro ambapo tutazifikia Halmashauri zote saba za Mkoa huu. Tumeanza na Wilaya ya Moshi Manispaa na Kata zake pamoja na Same kwa ajili ya uendelevu wa zoezi letu la kutoa Elimu ya Fedha kwa Umma, zoezi ambalo limeshafanyika katika Mikoa 13 na huu ni wa 14, na Mikoa mingine yote itafuata hadi Wananchi wote watakapofikiwa.” Alisema Bw. Kimaro.
Akizungumza wakati wa Semina hiyo alisema changamoto nyingi  zinatokana na uelewa mdogo wa Elimu ya Fedha na hasa katika masuala ya mikopo ambapo alisisitiza kuwa wananchi wanapaswa kufahamu kuwa kabla ya kukopa ni muhimu kuwa na malengo ya kukopa, kufahamu vyema watoa huduma watakao kwenda kukopa na kuwa na taarifa za kina ili kujua kama wamesajiliwa kwa mujibu wa Sheria na Kanuni lakini pia, ni muhimu kusoma na kuelewa mikataba ya watoa huduma ili wasije ingia katika matatizo ya mikopo kausha damu.
Bw. Kimaro aliongeza kuwa matarajio ya kutoa Elimu hiyo ni kuwa na wananchi wenye weledi katika masuala ya fedha na hivyo kuepuka kujiingiza katika biashara zisizo halali katika masuala ya fedha lakini kubwa zaidi ni kujenga utamaduni wa kujiwekea akiba, kuwekeza katika maeneo yenye tija na kukopa mahali palipo salama lakini pia kupanga mipango sahihi ya maisha baada ya kustaafu.
Elimu ya Fedha inayotolewa ni utekelezaji wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha wa miaka kumi kuanzia 2020/21-2029/30 pamoja na program ya Elimu ya Fedha kwa umma ya mwaka 2020/21 hadi 2025/26 ambapo imelenga kufikia 80% ya watanzania wote ifikapo 2025/26. 
Kwa sasa Wizara ya Fedha kupitia Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha imeshatoa Elimu ya Fedha katika Mikoa ya Kagera, Manyara, Singida, Tabora, Shinyanga, Lindi, Pwani, Mtwara, Morogoro, Rukwa, Arusha, na sasa inaendelea na kazi hiyo katika Mkoa wa Kilimanjaro.

About the author

mzalendoeditor