Featured Kitaifa

TANZANIA YAKABIDHIWA UENYEKITI KUNDI LA WATAALAMU MAJADILIANO MABADILIKO YA TABIANCHI BARA LA AFRIKA

Written by mzalendoeditor

Mshauri wa Rais, Masuala ya Mabadiliko ya Tabianchi na Mazingira Dkt. Richard Muyungi (kushoto) akizungumza jambo wakati wa mkutano wa Kundi la Wataalam wa Afrika la Majadiliano kuhusu mabadiliko ya Tabianchi (AGN) unaofanyika Nairobi nchini Kenya kuanzia Februari 10-12, 2025. Kulia ni Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kimataifa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Noel Kaganda.

Na Mwandishi Wetu,Nairobi, Kenya

Serikali ya Tanzania imekabidhiwa nafasi ya uenyekiti wa Kundi la Wataalam wa Afrika la Majadiliano kuhusu mabadiliko ya Tabianchi (AGN) kwa kipindi cha miezi tisa kuanzia Machi hadi Desemba, 2025.

Makabidhiano hayo yamefanyika jana Jumanne (Februari 11, 2025) katika Mkutano wa siku tatu wa Wataalam wa Afrika wanaoshiriki majadiliano hayo unaoendelea Jijini Nairobi nchini Kenya kuanzia tarehe 10- 12 Februari, 2025.

Nafasi hiyo ya Uenyekiti itaongozwa na Dkt. Richard Muyungi, ambaye ni Mshauri wa Rais Masuala ya Mabadiliko ya Tabianchi na Mazingira ambapo Tanzania itachukua jukumu hilo kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa jukwaa hilo mwaka 1995.

Makabidhiano hayo yamefanyika baina ya Mwenyekiti anayemaliza muda wake, Mhe. Balozi Ali Mohamed, kutoka Serikali ya Jamhuri ya Kenya na Mwenyekiti mpya Dkt. Richard S. Muyungi kutoka Tanzania.

Akizungumza mara baada ya makabidhiano hayo, Dkt. Muyungi alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kushiriki katika mijadala ya kutafuta suluhu zachangamoto zinazoikabili dunia ikiwemo ya masuala ya mabadiliko ya tabianchi.

“Rais Samia amejizolea sifa na kuiletea Tanzania heshima kubwa kimataifa na hiyo ni sababu mojawapo ya Tanzania kupewa heshima ya uongozi wa ndani ya jukwaa la AGN” amesema Dkt. Muyungi.

Aidha Dkt. Muyungi ametaja vipaumbele muhimu katika uongozi wake ni Pamoja na kuendelea kusukuma agenda ya mabadiliko ya tabianchi ikiwemo uhamasishaji wa matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mabadilko ya tabianchi katika kamisheni ya Umoja wa Afrika, Dkt. Hansen Nyambe, ameeleza kuwa uteuzi wa Tanzania kushika nafasi hiyo ni ushahidi wa juhudi kubwa zinazoendelea kufanywa na Mhe. Rais Dkt. Samia katika kuchagiza ajenda za Afrika katika kukabiliana na mabadilko ya tabianchi.

“Mhe. Rais Samia ni kinara wa upatikanaji wa nishati safi ya kupikia barani Afrika na dunia kwa ujumla, ambapo hivi karibuni aliongoza Wakuu wa Nchi za Afrika kujadili namna ya kufikisha umeme kwa watu milioni 300 wasiokuwa na nishati hiyo barani Afrika.

Watalaamu wa Mabadiliko ya tabianchi kutoka nchi 54 za Bara la Afrika na mashirika ya kimataifa wanakutana Jijini Nairobi kutathmini matokeo ya maamuzi ya mkutano wa 29 wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi uliofanyika nchini Azerbaijan, tarehe 11 hadi 22 Novemba 2024 na kuweka mikakati ya ufuatiliaji na utekelezaji. 

Aidha, mkutano huo una umelenga kuainisha vipaumbele vya Afrika katika Mkutano wa 30 wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi COP (30) utakaofanyika Novemba 2025 katika Mji wa Belem nchini Brazil.

Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo uliwakilishwa na Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kimataifa, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Noel Kaganda, na Kaimu Mkurugenzi Msaidizi masuala ya Mabadiliko ya Tabianchi na Tathmini, Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Kanizio  Manyika.

Mshauri wa Rais, Masuala ya Mabadiliko ya Tabianchi na Mazingira Dkt. Richard Muyungi (kulia) akiwa na Mwenyekiti wa Kundi la Wataalam wa Afrika la Majadiliano kuhusu mabadiliko ya Tabianchi (AGN) anayemaliza muda wake, Balozi Ali Mohammed kutoka Kenya (kushoto) pamoja na Mkurugenzi wa Idara ya Mabadiliko ya tabianchi na Uchumi wa Buluu Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Dkt. Hansen Nyambe (katikati) wakati wa mkutano wa AGN unaoendelea nchini Kenya, kuanzia Februari 10- 12, 2025.

Mshauri wa Rais, Masuala ya Mabadiliko ya Tabianchi na Mazingira Dkt. Richard Muyungi (wa pili kulia walioketi) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mkutano wa Kundi la Wataalam wa Afrika la Majadiliano kuhusu mabadiliko ya Tabianchi (AGN) unafanyika Jijini Nairobi nchini Kenya kuanzia Februari 10- 12, 2025.

 Mshauri wa Rais, Masuala ya Mabadiliko ya Tabianchi na Mazingira Dkt. Richard Muyungi (kushoto) akizungumza jambo wakati wa mkutano wa Kundi la Wataalam wa Afrika la Majadiliano kuhusu mabadiliko ya Tabianchi (AGN) unaofanyika Nairobi nchini Kenya kuanzia Februari 10-12, 2025. Kulia ni Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kimataifa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Noel Kaganda.

(NA MPIGAPICHA WETU)

About the author

mzalendoeditor