Featured Kitaifa

THBUB YATAKIWA KUWASISITIZA WATUMISHI WAKE KUZINGATIA MAADILI NA NIDHAMU YA KAZI

Written by mzalendo

Na MwandishiWetu, Dodoma.

Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Eliakim Maswi ameitaka Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) kuwasisitiza watumishi wote kufanya kazi kwa kuzingatia maadili na nidhamu ya kazi.

Maswi ameyasema hayo leo Februari 5,2025 Jijini Dodoma wakati akifungua mkutano wa 23 wa Baraza la Wafanyakazi wa Tume hiyo.

“Kama taasisi inayozingatia uzingatiaji wa haki za binadamu na misingi ya utawala bora, watumishi wa Tume lazima muwe mfano bora utakaoigwa na watumishi wengine wa umma ,”amesisitiza.

Amesema kuwa uwepo wa wajumbe hao katika baraza hilo ni kutokana na imani kubwa waliyopewa na watumishi wenzao ambao wamewachagua kuwawakilisha. Hivyo, wakirudi ofisini waeleze yale waliyokubaliana na utelezaji wake.

“Mimi napenda kila mtu ajue kile mlichokubaliana hapa kwa sababu kila idara ina mwakilishi wake,”amesema.

Pia, amesisitiza kuwa mikutano ya baraza la wafanyakazi itumike kujadili malengo, mipango ya taasisi ikiwa ni pamoja na maslahi ya watumishi.

Awali, Katibu Mtendaji wa THBUB na Mwenyekiti wa baraza hilo, Bw. Patience Ntwina amesema lengo la mkutano huo ni kupitia taarifa za utekelezaji wa kazi za Tume kwa mwaka 2024/2025 na kujadili mapendekezo ya mpango na bajeti kwa mwaka 2025/2026.

Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya watumishi wa THBUB Mwenyekiti wa Baraza la wafanyakazi (TUGHE) tawi la Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Bw. Pontian Kitorobombo amempongeza Katibu mkuu kwa kuwafungulia mkutano huo huku akiahidi kuwa watatumia muda huo kuwakilisha mawazo na changamoto za watumishi.

About the author

mzalendo