Featured Kitaifa

JAFO AUNDA KAMATI YA WATU 15 KUCHUNGUZA WAMACHINGA WA KIGENI WANAFANYA UMACHINGA KARIAKOO

Written by mzalendoeditor

 

WAZIRI wa Viwanda na Biashara Mhe.Dkt.Selemani Jafo, akizungumza na waandishi wa Habari jijini Dar es salaam wakati akitangaza timu ya watu 15 kwa ajili ya kutatua changamoto mbalimbali zilizopo katika Soko la Kariakoo  ili kuliwezesha kufanya kazi kwa ufanisi.

……….

Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe Dkt. Selemani Jafo ameunda Timu ya watu 15 kwa ajili ya kufuatilia changamoto inayowakumba wafanyabiashara wa Kariakoo ya wawekezaji wageni wanaokuja nchini na ajenda ya uwekezaji kinyume chake wanajishughulisha na biashara za rejereja (Wamachinga) na kuathiri uchumi wa wafanyabiashara wazawa.

Dkt. Jafo alitangaza Timu hiyo  jijini Dar es Salaam wakati akiongea na Uongozi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Kariakoo ambapo kuhusu utatuzi wa Changamoto mbalimbali zilizopo katika Soko hili ili kuliwezesha kufanya kazi kwa ufanisi.

Dkt Jafo alifafanua kuwa Timu hiyo inayojumuisha wajumbe kutoka Taasisi mbalimbali katika sekta ya umma na binafsi itafanya kazi kwa siku 30 na itaanza kazi hivi karibuni ikiongozwa na Mwenyekiti wao Edda Tandi Luoga Mkuu wa Chuo cha Elimu ya biashara (CBE)

Aidha, Dkt. Jafo akieleza majukumu ya timu hiyo amesema Timu hiyo inatakiwa kufanya utafiti kwa kina kwa soko la kariakoo, kubaini ukubwa wa tazizo la wageni kupewa vibali na leseni za kufanya biashara nchini zinazoweza kufanywa na watanzania, kuchambua uhalali wa vibali na leseni zilizotolewa kwa wafanyabiashara wageni.

Aidha Dkt Jafo amesema Timu hiyo itafanya kazi ya kubaini sekta na aina ya biashara na maeneo yenye changamoto kwa wageni hapa nchini, kuchunguza utaratibu na upatikanaji wa nyumba za kufanyia biashara kwa wageni, kuchunguza udhaifu wa mfumo na uwezekano wa wageni kutumia njia zisizo rasmi kufanya biashara hapa nchini,

Aidha, Timu hiyo inatakiwa kutoa mapendekezo ya hatua za haraka zitakazoweza kuchukuliwa na taasisi katika kudhibiti wageni wanaoingia kufanya biashara na ajira zinazostahili kufanywa na Watanzania.

About the author

mzalendoeditor