Featured Kitaifa

SERIKALI KUIMARISHA MIKAKATI YA KUKUZA SHUGHULI ZA UKUZAJI VIUMBE MAJI ZIWA TANGANYIKA

Written by mzalendo

Serikali imeendelea kufanya juhudi za kuimarisha na kuweka mikakati bora ya kukuza shughuli za Ukuzaji Viumbe maji kupitia vizimba vya kufugia samaki ambapo njia hii inalenga kuboresha zaidi Uzalishaji wa Samaki na kukuza shughuli za uchumi kwa wananchi na kufungua fursa za uchumi.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, leo Januari 22, 2025 mkoani Dodoma katika Mkutano wa kujadili ni namna gani ya kuimarisha Tasnia ya Ukuzaji Viumbe Maji kwa njia ya Vizimba na mashirikiano baina ya Wizara na Shirika la Uhifadhi wa Mazingira “The Nature Conservancy” pamoja na Taasisi zingine, Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji, Dkt. Nazael Madalla amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alielekeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuhakikisha inahamasisha na kuendelea Ufugaji Samaki kwa njia ya Vizimba katika maeneno yote yanayofaa kiufugaji.

“hapa nchini kwetu Ziwa Tanganyika ni moja ya maeneo ambayo kuna fursa ya Ufugaji Samaki kwa njia ya Vizimba, na tumekutana hapa na wadau mbalimbali wa Ufugaji Samaki kwa njia ya Vizimba kutoka ndani ya nchi na nje ya nchi kwa ajili ya kujadili ni namna gani tutawezesha Ufugaji huu kwa jamii inayozunguka Ziwa Tanganyika, na kukubaliana kwa mikakati kuhakikisha kwamba kunakuwa na uwezeshaji pamoja na ulinzi wa mazingira na utunzaji wa mazingira hayo ili kuleta faida nchini.” amesema Dkt. Madalla

Aidha, Dkt. Madalla amesema serikali imekuwa ikifanya juhudi katika kukuza Tasnia ya Ukuzaji Viumbe Maji kwani tayari ilishapeleka Vizimba katika Ziwa Tanganyika na jana Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji alikwenda kutembelea Vizimba hivyo ambavyo vipo katika eneo la Katavi ambavyo wafugaji tayari walishaanza kufuga na Samaki wanaendelea vizuri kiasi cha kuwatia moyo wafugaji hao.

Vilevile Dkt. Madalla amesema Serikali kupitia Wizara inaendelea na zoezi la kutoa mafunzo kwa wavuvi juu ya Ufugaji Samaki kwa njia ya Vizimba, kutoa mikopo ya pembejeo, kuendeleza maeneo ya Ufugaji, kuanza Taratibu za kuanzisha Kituo cha Ukuzaji Viumbe Maji katika Ziwa Tanganyika, pamoja na kuhamasisha na kuwezesha Sekta Binafsi ili kuwekeza katika Uzalishaji na usambazaji wa pembejeo za Ufugaji Samaki.

Dkt. Madalla amesema kuwa kwa sasa mwitikio wa wananchi kufuga samaki kwa njia ya vizimba umeanza kuongezeka kutokana na serikali kuweka mazingira rafiki ikiwemo mikopo ambayo imekuwa ikiwanufaisha sana wafugaji wengi na baaadhi ya wadau katika Sekta wameainisha ni kwa namna gani ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba ulivyokuwa na tija kubwa kiuchumi kwani kwa sasa wananufaika sana kutokana na mradi huo.

Naye, Mkurugenzi wa Uvuvi kutoka Mamlaka ya Ziwa Tanganyika (LTA), Bi. Nyakorema Beatrice Marwa, amesema warsha hii inatija kubwa sana kwa sababu imekusanya wadau mbalimbali wa Tasnia ya Ukuzaji Viumbe Maji toka Taasisi za Serikali na Binafsi na wadau wa Ziwa Tanganyika na lengo kutaka kuanda Mpango wa Utekelezaji kwa pamoja ambao haukizani na Sheria zetu na za nchi nne zinazozunguka Ziwa Tanganyika.

Pia, Meneja wa Mradi wa Ziwa Tanganyika wa Shirika la Uhifadhi wa Mazingira “The Nature Conservancy” (TNC), Bw. Fridolin Nzambimana amesema kuwa TNS wanachokifanya ni kuimarisha mashirikiano baina yao na serikali pamoja na Taasisi nyingine ili kuendeleza na kukuza Tasnia ya Ukuzaji Viumbe maji kwa njia ya kutumia Vizimba na ambayo inalinda rasilimalinza Uvuvi.

About the author

mzalendo