Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji ameagiza kufungwa kwa viwanda na maduka yote yanayojihusisha na Nyavu zisizofaa kwenye shughuli za Uvuvi ikiwa ni hatua ya kukomesha Uvuvi haramu nchini.
Mhe. Kijaji amesema hayo leo Disemba 19, 2024 wakati wa ziara yake mkoani Mara baada ya kupokea taarifa ya Utekelezaji wa Shughuli za Uvuvi mkoani humo iliyobainisha kwa kiasi kikubwa changamoto ya Uvuvi haramu.
“Hizi nyavu na nyenzo nyingine za Uvuvi haramu kuna mahala zinatengenezwa na kuuzwa ndipo zinawafikia wavuvi wetu hivyo ni lazima tuanzie huko kwenye msingi kabla hatujawashughulikia wavuvi” Amesema Mhe. Dkt. Kijaji.
Mhe. Dkt. Kijaji amebainisha kuwa moja ya jukumu lake kubwa wakati wote atakaohudumu kwa nafasi yake ni kuhakikisha anarejesha hali ya upatikanaji wa samaki nchini kama ilivyokuwa awali ili kuokoa viwanda vya kuchakata samaki vilivyopo nchini hivyo mbali na hatua hiyo ameweka wazi kuwa wanakusudia kudhibiti uingizwaji wa zana hizo kwenye mipaka huku wakianza na mpaka wa Tunduma.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Mtambi ametangaza awamu nyingine ya kupambana na Uvuvi haramu mkoani humo itakayoanza mwezi Januari mwakani ambapo amewataka wale wote wanaojihusisha na vitendo hivyo kuacha mara moja huku akiwatahadharisha kutomlaumu pindi atakapoanza kutekeleza operesheni hiyo.
“Mtu anayefanya vitendo vya Uvuvi haramu ni mhujumu na sisi jeshi mhujumu “hatumpetpet” bali tunamshughulikia ipasavyo” Amesisitiza Mhe. Kanali Mtambi.
Mhe. Dkt. Kijaji amefanya ziara yake ya kwanza kikazi mkoani Mara tangu alipoapishwa kushika wadhifa huo ambapo amefanya vikao kazi na wataalam na watendaji wa Serikali mkoani humo na kutembelea vizimba vya kufugia samaki vilivyotolewa na Serikali kwa mkopo wa masharti nafuu kwenye eneo la Lake Side.