Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Dkt. Festo Dugange(Mb) amesema ujenzj wa soko kuu la mazao ya nafaka eneo la Kanondo Wilayani Sumbawanga Mkoani Rukwa ni Mkombozi wa wakulima kwani Soko hilo litaongeza thamani ya mazao na kukuza mzunguko wa fedha mkoani humo.
Mheshimiwa Dkt Dugange amesema hayo wakati wa hafla ya utiaji saini mkataba wa ujenzi wa soko kuu la mazao iliyofanyika leo Disemba 6, 2025 katika ukumbi wa Nazareti Manispaa ya Sumbawanga, Rukwa.
Ujenzi wa soko hilo ni miongoni mwa miradi inayotekelezwa na Mradi wa uboreshaji miji nchini Tanzania (TACTIC) ambapo jumla ya shilingi Bilioni 7.4 zinatarajiwa kutumika katika ujenzi wa soko hilo unaotarajiwa kukamilika Disemba 2025 ikijumuisha ujenzi wa eneo la kuuzia, kuandalia, kukaushia na kuchambua ili kuweka katika makundi ya ubora pamoja na eneo la maghala ya kuhifadhia mazao mbalimbali ya nafaka.
“Soko hili la kisasa limekuja kwa wakati sahihi kwasababu wananchi wa Mkoa wa Rukwa ni wakulima wakubwa na wachapakazi sana, wanalisha Taifa letu, wanalisha na nchi jirani hasa kwa zao la mahindi na mazao mengine ndio maana Mhe. Rais aliona akasema lazima awaletee fedha za kujenga soko la kisasa la mazao ili tuweze kuhifadhi mazao yetu kwa ubora zaidi, tuondoe upotevu na uharibifu wa mazao unaotuletea hasara lakini pia kuongeza thamani ya mazao yetu,” alisema Mhe. Dugange.
Katika hatua nyingine, Dkt. Dugange amesema Wizara ya TAMISEMI itahakikisha inasimamia vyema matumizi ya fedha za mradi huo pamoja na ubora wa miradi yote ya TACTIC ili kuhakikisha thamani ya fedha inaonekana, akiwataka Wakurugenzi wote wa Halmashauri zenye miradi ya TACTIC kuhakikisha kuwa miradi hiyo inakamilika kwa wakati ili kuharakisha tija kwa wananchi.
Aidha Mhe. Dugange ametumia sehemu ya hotuba yake kuwataka Viongozi wa serikali za Mitaa kwenye maeneo yote 45 yanayotekeleza miradi ya TACTIC kuhamasisha na kuelekeza wananchi kutumia vyema miradi hiyo ili kujipatia faida zaidi na kuongeza pato binafsi kupitia shughuli mbalimbali za kiuchumi kwenye maeneo yao.