Featured Kitaifa

RC DODOMA AWAITA WANANCHI KUJITOKEZA KWA WINGI KATIKA ZOEZI LA UBORESHAJI WA DAFTARI LA KUDUMU

Written by mzalendoeditor

Mkuu wa Mkao wa Dodoma Rosemary Senyamule, akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 24,2024 wakati akitoa taarifa kuhusu zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura linalotarajia kuanza Septemba 25 hadi Oktoba 1,2024.

Na Gideon Gregory, Dodoma.

Wakazi wa Mkoa wa Dodoma wametakiwa kujitokeza kwenye zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura litakaloanza kesho kwa siku saba hadi Oktoba Mosi mwaka huu.

Akizungumza leo Septemba 24,2024 na waandishi wa habari jijini Dodoma Mkuu wa Mkao wa Dodoma Rosemary Senyamule amesema wahusika kwenye uboreshaji huo ni wananchi waliotimiza miaka 18 na watakaotimiza umri wa miaka 18 kabla tarehe ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

“Uboreshaji huu ni sehemu ya mchakato na utahusisha kurekebisha taarifa, uandikishaji wa wapiga kura wapya na kuwaondoa kwenye daftari waliokosa sifa kwamfano waliofariki, waliofungwa vifungo vya zaidi ya miezi Sita na sababu nyingine muhimu ili kuhakikisha wapiga kura wanahakiki taarifa zao,”amesema.

Amesema ni muhimu wapiga kura kuhakikisha wanataarifa sahihi ili waweze kutimiza haki yao ya kikatiba katika uchaguzi ujao wa mwaka 2025.

Aidha, ametaja vituo vitakavyotumika katika uboreshaji huo kuwa ni majengo ya umma kama vile Ofisi za Watendaji wa Kata, Mitaa,Wenyeviti wa Vijiji,Vitongoji, shule na maeneo ambayo hakuna majengo ya umma vituo vimeshajengwa na kuwekwa alama ili wananchi kuvitambua.

“Idadi ya vituo ni kama ifuatavyo kwa kila Wilaya ambapo Wilaya ya Dodoma vituo 429, Bahi 191, Kongwa 229 na Chamwino 805, Aidha wanaohusika katika zoezi hili ni wananchi wote waliotimiza umri wa miaka 18 na kuendelea, waliojiandikisha awali na wamehama Kata au Jimbo moja kwenda jingine au waliopoteza sifa wanatakiwa kuondolewa pamoja na waliopoteza kadi na kukosea taarifa zao wakati wa kujiandikisha, “amesema.

Mkoa wa Dodoma unakadiriwa kuwa na wapiga kura 1,777,834 kati ya hao wapo ambao hawajawahi kujiandikisha idadi yao inakadiriwa kuwa 845,976.

About the author

mzalendoeditor