Featured Kitaifa

NGOs ZINGATIENI VIPAUMBELE VYA SERIKALI KUTEKELEZA MIRADI: NAIBU WAZIRI MWANAIDI

Written by mzalendo

Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Mwanaidi Ali Khamis ameyasisitiza Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini kuzingatia malengo, mipango, mikakati na vipaumbele vya Taifa katika utekelezaji wa miradi.

Naibu Waziri Mwanaidi ameyasema hayo wakati akifunga mafunzo kwa Wasajili wasaidizi wa NGOs na Wajumbe wa Baraza la Taifa la NGOs (NaCONGO) Septemba 05, 2024 jijini Dodoma.

Amesema utekelezaji wa shughuli za Mashirika Yasiyo ya Kiserikali unapaswa kuzingatia sio tu sheria, kanuni na miongozo ya uratibu wa Mashirika hayo, bali na matakwa ya sheria nyingine za nchi kama ilivyoainisha katika Kifungu cha 21(a) cha Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Sura ya 56 ya Sheria za Tanzania.

“Ikumbukwe kwamba, uzingatiaji wa misingi ya sheria, kanuni na miongozo wakati wa utekelezaji wa shughuli za Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, ndio msingi wa utambuzi wa mchango wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika nyanja mbalimbali na Taifa kwa ujumla,” amesema Naibu Waziri Mwanaidi

Ameongeza kwamba, ushirikiano kati ya Wizara na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kupitia Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO) yanaweka Mazingira rafiki na wezeshi ya utendaji kazi wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, pamoja na kuimarisha mifumo ya ubadilishanaji wa taarifa katika kuwahudumia wananchi.

“Napenda kuwapongeza kwa ushiriki wenu mzuri katika mafunzo na majadiliano haya tangu yalipofunguliwa. Aidha, ninawaomba mkazingatie miiko ya utekelezaji wa majukumu yenu sawasawa na sheria mbalimbali za nchi kwa lengo la kuuza Sekta ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na Taifa kwa jumla,” amesisitiza Naibu Waziri Mwanaidi

Jukwaa la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kwa mwaka 2024 linatarajiwa kutimishwa Septemba 06, 2024 jijini Dodoma na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko likiongozwa na Kaulimbiu; Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ni Wadau Muhimu, Washirishwe Kuimarisha Utawala Bora.”

About the author

mzalendo