Featured Kitaifa

WANA MAHENGE WATAKIWA KUCHANGAMKIA FURSA ZITAKAZOWAINUA KIUCHUMI

Written by mzalendo


Afisa Maendeleo ya Jamii, Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga Mjini Mahenge Bw. Peter Nambunga, akiongea na washiriki waliohudhuria program maalum ya elimu ya fedha kwa umma iliyofanyika katika Halmashauri hiyo Mkoani Morogoro.

Mratibu wa Mifuko na Program za Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kutoka Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Bw. Samwel Shikona, akiwaeleza wananchi wa Mahenge fursa mbalimbali zinazopatikana kupitia Baraza hilo wakati wa program maalum ya elimu ya fedha kwa umma iliyotolewa kwa wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga.

Afisa Usimamizi wa Fedha kutoka Wizara ya Fedha, Bw. Stanley Kibakaya, akiwaeleza wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga naomna bora ya kuepukana na mikopo isiyo rasmi (mikopo umiza) wakati wa program maalum ya elimu ya fedha kwa umma iliyotolewa kwa wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga.

Afisa Sheria Mwandamizi kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw Ramadhani Myonga, akitoa mada kwa wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro, wakati wa program maalum ya elimu ya fedha kwa umma iliyotolewa kwa wananchi wa Halmashauri hiyo..

Mjasiriamali na mtangazi wa Radio Ulanga FM, Easter Kaonja akichangia mojawapo ya mada iliyotolewa kwenye program maalum ya elimu ya fedha kwa umma iliyotolewa kwa wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga.

Wataalamu wa masuala ya fedha kutoka Wizara ya Fedha na washirika wa sekta ya fedha nchini wakiwa katika picha ya pamoja na Maafisa Maendeleo ya Jamii pamoja na wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga mara baada ya program ya elimu ya fedha kwa umma iliyotolewa kwa wananchi hao.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha – Morogoro)

Na. Ramadhani Kissimba, WF, Morogoro

Wananchi wa Mahenge katika Halmashauri ya Wilayani ya Ulanga, Mkoani Morogoro wametakiwa kuchangamkia fursa zinazotolewa na Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) ili waweze kujikwamua kutoka katika lindi la umasikini kwa kuongeza kipato na kukuza uchumi.

Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga, Bw. Peter Nambunga, alisema hayo katika program maalum ya elimu ya fedha kwa umma iliyotolewa kwa wananchi wa Mahenge na wataalamu kutoka Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na washirika wa sekta ya fedha nchini ikiwa ni mwendelezo wa kutoa elimu hiyo kwa nchi nzima hasa kwa wananchi waliopo vijijini.

Bw. Nambunga alieleza kuwa elimu iliyotolewa itajenga uelewa mkubwa kwa wananchi tunaowasimamia kwa maana imelenga kuikwamua jamii kiuchumi.

Bw. Nambunga aliongeza kuwa wananchi wa Mahenge na Tanzania kwa ujumla wanatakiwa kuzitumia fursa zaidi ya 72 zinazotolewa na Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi katika kuendeleza shughuli zao mbalimbali za uzallishaji mali ili kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja na jamii kwa ujumla na kusaidia kupeleka mbele gurudumu la maendeleo.

‘’Wananchi wameweza kuelewa fursa mbalimbali zinazopatikana kupitia Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, wengi wao walikuwa wanajikita na kuelewa uwezeshaji wananchi kiuchumi ni ile mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri lakini leo wametambua kuwa kuna mifuko zaidi ya 72 ambayo wanaweza kuitumia kupata uwezeshaji katika suala zima la maendeleo’’. Alisema Bw. Nambunga

Aidha, Afisa Maendeleo ya Jamii huyo aliwataka wananchi wa Mahenge na Halmashauri nzima ya Ulanga kuwa na nidhamu katika matumizi ya fedha ili kuwaepusha na uhitaji wa kutafuta mikopo isiyo ya lazima na kwa kufanya hivyo itakuwa njia mojawapo ya kuepukana na mikopo ya kausha damu.

Awali akizungumza katika program hiyo, Mratibu wa Mifuko na Program za Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kutoka Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Bw. Samwell Shikona, alisema kuna fursa mbalimbali za kuwakomboa wananchi kiuchumi zikiwemo mikopo kwa wakulima ambayo ina masharti nafuu, lakini kuna mikopo nafuu inayotolewa kwa wakulima ambao wana umri kati ya miaka 18 hadi 40 ambayo haina masharti yoyote.

Bw. Shikona aliwataka vijana kuchangamkia fursa hiyo ya mikopo ya kilimo ambayo itawasaidia kuondokana na utegemezi kwa kuwakomboa katika kuingia kwenye umasikini.

Aidha alieza kuwa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi lipo kwa ajili ya kuwaunganisha wananchi na fursa mbalimbali za kiuchumi kwa lengo la kuongeza kipato chao ili waweze kuchangia pato la Taifa.

Program ya elimu ya fedha kwa umma inayotolewa na Serikali kupitia Wizara ya Fedha na washirika kutoka sekta ya fedha nchini ina malengo mahsusi la kuwaunganisha wajasiriamali na fursa mbalimbali zinazotolewa na sekta ya fedha katika kukuza na kuimarisha biashara zao.

About the author

mzalendo