Featured Kitaifa

WAZAZI PELEKENI VIJANA WENU SHULE – MAJALIWA

Written by mzalendo

 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na  wananchi wa kijiji cha Mtondo, Kata ya Nambilanje wilayani Ruangwa, mkoa wa Lindi, Agosti 22, 2024.  ( Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwapungia  wananchi wa kijiji cha Mtondo, Kata ya Nambilanje wilayani Ruangwa, mkoa wa Lindi alipowasili kijijini hapo kuzungumza nao, Agosti 22, 2024.( Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Salim Abdallah Nampota alipowasili katika kijiji cha Mtondo, Kata ya Nambilanje wilayani Ruangwa, mkoa wa Lindi  kuzungumza na wananchi, Agosti 22, 2024.

 

 Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wazazi wahakikishe vijana wao wanakwenda kusoma kwenye shule za sekondari kwani bila elimu hawawezi kufika mbali.

“Wazazi wenzangu hakikisheni vijana wenu wanaenda shule. Hatuwezi kufika mbali kama vijana wetu hawaendi shule. Tunajenga shule kila mahali, tunataka maeneo yote yawe na shule,” alisema.

Waziri Mkuu Majaliwa ambaye pia ni Mbunge wa Ruangwa alitoa kauli hiyo jana (Alhamisi, Agosti 22, 2024) wakati akizungumza na wakazi wa kijiji cha Mtondo, Kata ya Nambiranje, Ruangwa mkoani Lindi.

Akielezea hatua iliyofikiwa kutokana na juhudi za Serikali ya awamu ya sita, Waziri Mkuu alisema Wilaya ya Ruangwa imepiga hatua kwenye sekta za elimu, maji na afya ikilinganishwa na hali ilivyokuwa miaka ya nyuma.

Alisema wilaya hiyo ina shule tatu za wasichana pekee ambazo ni Liuguru, Ruangwa Girls na Lucas Malia. “Vilevile tumefanikiwa kujenga shule za sekondari zenye kidato cha tano na sita ambazo ni Ruangwa, Mbekenyera, Nkowe, Lucas Malia na Hawa Mchopa. Shule ya sita ya Mandawa itakamilika hivi karibuni,” alisisitiza.

Akielezea utekelezaji kwenye sekta ya maji, Waziri Mkuu alisema vijiji vyote 90 vya wilaya vilichimbiwa maji kupitia taasisi ya GAIN lakini kwa sasa hayatoshi. Hata hivyo, alitumia fursa hiyo kuwajulisha kwamba Serikali imetoa sh. bilioni 49 kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa maji kutoka Nyangao ambao utavinufaisha vijiji 34 vya wilaya ya Ruangwa na vijiji 29 vya wilaya ya Nachingwea.

Kuhusu umeme, alisema kwamba laini zimeshaenda kwenye kila kijiji na kwamba Serikali hivi sasa inashughulika kuweka umeme kwenye ngazi ya vitongoji. “Leo hii hakuna kijiji kisichokuwa na umeme.”

Kuhusu barabara, alisema kuna changamoto ya barabara kufika katika kijiji cha Mtondo ambayo tayari iko kwenye mpango wa ujenzi. “Kuna barabara ya kutoka Mandawa Chini hadi hapa, Nanjalu hadi hapa, Nambiranje hadi hapa na kutoka Namiyenje hadi hapa.”

Mapema, Diwani wa Kata ya Nambiranje, Mossa Mohammed Mtejela alimuomba Waziri Mkuu awasaidie ili waongezewe fedha za ujenzi wa barabara ya kutoka Mtondo hadi Mkaranga Sekondari yenye urefu wa kilometa saba kwa sababu kuna daraja linapaswa kujengwa na fedha iliyotengwa ni sh. milioni 300 tu.

“Tunaomba utusaidie ili tuongezewe fedha za ujenzi wa barabara ya Mtondo hadi Mkaranga Sekondari na daraja la mto Moha kwenye kijiji cha Mkaranga. Shilingi milioni 300 zilizotolewa haziwezi kutosha,” alisema.

Pia aliomba wajengewe bweni la wavulana kwenye sekondari ya Nambiranje kwa sababu kuna baadhi ya wanafunzi wanatembea km.7.5 kutoka Mtondo na wengine km. 16 kutoka Nanjalu. “Tunaomba tujengewe bweni ili kuwasaidia watoto wetu lakini pia kupunguza utoro wa rejareja,” alisema.

Shule hiyo ya kata tayari ina bweni moja la wasichana lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 80.

Waziri Mkuu anaendelea na ziara jimboni kwake.

About the author

mzalendo