Featured Kitaifa

KAMATI YA BUNGE YAIPONGEZA NDC NA SIDO KWA UTENDAJI

Written by mzalendoeditor

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo imelipongeza Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) kwa usimamizi mzuri wa Miradi ya kimkakati ya Kitaifa na
Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) kwa kuwawezesha wajasiliamali wadogo wadogo kukuza biashara.

Kamati hiyo imeyataka Mashirika hayo kutekeleza shughuli zake kwa ufanisj na kuongeza kuongeza uwigo wa utoaji huduma kwa kuwa ni Mashirika muhimu katika kukuza biashara , kuongeza ajira na pato la Taifa kwa ujumla.

Kamati hiyo ikiongozwa na Mwenyekiti wake Mhe. Deodatus Mwanyika ( Mb) ineyapongeza Mashirika hayo yaliyoko chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara wakati wa uwasilishaji wa Taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Mashirika hayo kwa Kamati hiyo Agosti 14, 2024 katika ukumbi wa Bunge Jijini Dodoma.

Aidha, Wajumbe wa Kamati hiyo walipata fursa ya kutoa maoni mbalimbali yaliyolenga kuboresha utendaji kazi wa Mashirika hayo ili yaweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, kupunguza uagizaji wa bidhaa nje ya nchi, kutoa huduma kwa gharama nafuu kwa wajasiriamali, kuvutia wawekezaji, kuongeza ajira kwa vijana na pato la Taifa kwa ujumla

Naye, Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Selemani Jafo
akiwa ameambatana na
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe Exaud Kigahe (Mb.), Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda Bw. Needpeace Wambuya,
ameihakikishia Kamati hiyo kuwa Wizara yake itayafanyia kazi maoni na mapendekezo yote yaliyotolewa na kuahidi kushirikiana na Kamati hiyo katika kuendeleza jitihada mbalimbali na programu Maalum za kuendeleza Sekta ya Viwanda na Biashara.

Naye, Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) Dkt. Nicolaus Shombe akitoa elimu kwa wajumbe hao amesema NDC inatekeleza miradi ya kielelezo (Flagship projects) ambapo inefanikiwa kulipia fidia wananchi kupisha Mradi unganishi wa Mchuchuma na Liganga na kusaini Mkataba wa Uchimbaji Madini ya Chuma Maganga Matitu,

Aidha amebainisha kuwa NDC imefanikiwa kuzalisha
bidhaa za kibailojia zisizo na kemikali ikiwemo viuadudu vya kuua viluwiluwi wa mbu wanaoeneza ugonjwa wa malaria na magonjwa mengine yanayoambukizwa na mbu, viatilifu hai vya kuua wadudu waharibifu kwenye mazao na mbolea hai na kuuza ndani na nje ya nchi.

Awali, akitoa taarifa ya utendaji kwa Shirika hilo kwa Kamati hiyo, Mkurugenzi wa SIDO Mhandisi Prof. Sylvester Mpanduji alieleza kuwa SIDO imeendelea kutekeleza majukumu yake kwa kutoa huduma za kiufundi na maendeleo ya teknolojia, Uanzishaji wa miradi ya viwanda vidogo vijijini, Mafunzo, Ushauri na huduma za ugani, Masoko na Habari, na Huduma za fedha kwa wajasiliamali wadogo.

Pia, amesema SIDO imejipanga kutanua uwigo wa utuoaji huduma inayopatikana katika mikoa yote na kuelekeza huduma hizo katika kila wilaya ili kuongeza kasi ya uanzishaji na ukuzaji wa viwanda vidogo nchini ambavyo vitaongeza ajira na kukuza biashara na uchumi wa nchi.

About the author

mzalendoeditor