Featured Kitaifa

MAKUNDI MBALIMBALI YAMIMINIKA BANDA LA KAMPENI YA MSAADA WA KISHERIA YA MAMA SAMIA DODOMA

Written by mzalendoeditor

Wataalamu wa sheria wakitoa elimu ya msaada wa kisheria kwa wananchi waliofika kwenye banda la Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia kwenye maonesho ya nanenane jijini Dodoma

Na Mwandishi Wetu, DODOMA

IKIWA kesho ni kilele cha maonesho ya nanenane yanayofanyika kitaifa Dodoma, maelfu ya wananchi ikiwamo vikundi vya vikoba wameendelea kujitokeza kupatiwa elimu na huduma ya msaada wa kisheria kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia.

Akizungumza katika banda la kampeni hiyo lililopo chini ya Wizara ya Katiba na Sheria leo, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Msaada wa Kisheria wa Wizara hiyo, Ester Msambazi amesema idadi kubwa ya wananchi kwa siku nne za maonesho wamejitokeza kupata elimu na kusikilizwa migogoro yao ya kisheria.

“Tangu Agosti mosi hapa viwanja vya nanenane tunatoa huduma na huduma tunazozitoa ni pamoja na ushauri wa kisheria, kumuandalia mwananchi nyaraka za kisheria ili awasilishe mahakamani lakini pia tunatoa elimu kwa makundi mbalimbali ikiwamo wanafunzi, vikundi vya wanawake kama vikoba.”

“Tunawapa elimu ya masuala mbalimbali lakini pia tunasikiliza migogoro ya mtu mmoja mmoja hadi sasa tumesikiliza migogoro 26 inayohusu masuala ya ardhi, mirathi, ndoa , matunzo ya watoto na migogoro mingine,”amesema.

Ametoa rai kwa wananchi wa Mkoa wa Dodoma na mikoa Jirani wafike katika banda la Wizara ya Katiba na Sheria ili kupata huduma za msaada wa kisheria kupitia hiyo kampeni hiyo.

Hata hivyo, amewataka waliopo nje ya Dodoma kufika kwenye mashirika yanayotoa huduma za msaada wa kisheria katika maeneo yao ili waweze kupata huduma za msaada wa kisheria kulekule waliko na kama hawafahamu wafike ofisi za Halmashauri za Wilaya na Mji watapata maelekezo.

“Wananchi watumie fursa hii ambayo Mama (Rais Samia) ametupatia kama wananchi tusiokuwa na uwezo wa kumudu gharama za mawakili, hadi sasa katika mikoa saba tumefikia wananchi zaidi ya 493,000 wakijumuishwa wanawake, watoto, makundi maalum wanaume na tumetatua migogoro mbalimbali,”amesema.

Pia amesema wamesajili vyeti vya kuzaliwa kupitia taasisi ya RITA na huduma mbalimbali zimetolewa ikiwamo namna ya kuandaa wosia.

“Wizara imejipanga kuhakikisha kampeni hii inatekelezwa katika mikoa yote ya Tanzania, wananchi 266,000 wamehudumiwa idadi hii ni kubwa kwa hizi siku nne ambazo tumeanza na tunatarajia kuhudumia wananchi wengi zaidi, kama Wizara tumejipanga wapo wanasheria wa Wizara ya Katiba na Sheria, Ofisi ya Mwendesha Mashtaka, Mkoa wa Dodoma, tumejipanga kuhudumia wananchi,”amesema.

Awali, amefafanua kuwa wizara inaratibu na kusimamia watoa huduma za msaada wa kisheria ikiwa na lengo la kuhakikisha kwamba huduma za msaada wa kisheria zinapatikana kwa wananchi ili wale wasioweza kuifikia haki kwa kukosa uwezo wa kumudu gharama za mawakili sasa waifikie haki kupitia huduma za msaada wa kisheria.

“Katika kuhakikisha kwamba wananchi wanafahamu huduma hizi za msaada wa kisheria wizara inatekeleza kampeni maalum kabambe ya huduma za msaada wa kisheria inayoitwa Kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia,”amesema.

Amesema kampeni hiyo inatekelezwa katika ngazi za jamii na hadi sasa imetekelezwa katika mikoa hiyo saba na wanatumia majukwaa, maadhimisho na maonesho mbalimbali kufikia wananchi.

Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Msaada wa Kisheria wa Wizara ya Katiba na Sheria, Ester Msambazi akizungumza na waandishi wa habari kuhusu huduma inayotolewa na Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia katika viwanja vya nanenane jijini Dodoma.

Wataalamu wa sheria wakitoa elimu ya msaada wa kisheria kwa wananchi waliofika kwenye banda la Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia kwenye maonesho ya nanenane jijini Dodoma

About the author

mzalendoeditor