Na Avelina Musa – Dodoma
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe,Rosemary Senyamule ameipongeza Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu Tanzania kwa kuendelea kuziunga mkono Juhudi za Mhe,Rais Samia kwa kuhamasisha jamii kuhusu Utalii katika maeneo ya Bahari na Uchumi wa Buluu Nchini.
Mhe,Senyamule amesema hayo Leo Agosti 4.2024 alipotembelea banda la Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu Tanzania katika Maonyesho ya Kitaifa ya Wakulima na wafugaji nane nane (88) Jijini Dodoma.
“Niwapongeze kwa kazi nzuri mnayoifanya kwa kuendelea kuihamasisha jamii kuhusu utalii wa bahari na uchumi wa buluu kwani kwa kufanya hivyo mnaziunga mkono juhudi za Mhe,Rais katika kutangaza vivutio vyetu,”alisema Senyamule.
Kwa Upande wake Afisa Masoko kutoka Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu Tanzania bi,Halima Tosiri amesema hicho ni kitengo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi chenye dhamana ya kusimamia na kuendeleza Rasilimali za Bahari.
Aidha Bi,Halima amesema Lengo la ushiriki wao katika maonesho hayo ni kuwaonyesha Watanzania shughuli zinazofanyika ndani ya Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu Tanzania na kuhamasisha Utalii katika maeneo ya bahari na uchumi wa buluu Nchini.
“Nitumie nafasi hii kuwaalika watu wote kufika katika Banda letu lililopo katika hema la Wizara ya Mifugo na Uvuvi ili wajifunze shughuli zinazofanywa na Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu Tanzania”alisema Halima.