Featured Kitaifa

RHMT’s & CHMT’s ZATAKIWA KUWAJIBIKA KATIKA TAALUMA ZAO

Written by mzalendo

Mkurugenzi wa Huduma za Afya,Ustawi wa Jamii na Lishe Ofisi ya Rais – TAMISEMI Dkt. Rashid Mfaume amezitaka Timu za Usimamizi wa Shughuli za Afya za Halmashauri (CHMTs) na mkoa (RHMTs) nchini kuwajibika katika taaluma zao katika kusimamia huduma na ujenzi wa miradi katika maeneo ya kutolea huduma Afya.

Dkt. Mfaume ametoa maelekezo hayo akiwa katika Hospitali ya Halmashauri ya wilaya ya Songea baada ya kutoridhishwa na utendaji wa CHMT ya Halmashauri hiyo kwa kutosimamia eneo la utoaji wa huduma za Afya pamoja na ujenzi wa miundombinu ya kutolea huduma ikiwemo jengo la maabara ambalo taarifa ya hospitali ilitaja kukamika kwa ujenzi ili hali jengo hilo halijakamilika.

“CHMT ya Songea DC na DMO wake wameamua kuidanganya Ofisi ya Rais -TAMISEMI achilia mbali kutowajibika katika kuandaa taarifa lakini pia usimamizi wa timu sio mzuri kwahiyo, tunaomba mkurugenzi awaandikie barua pamoja na DMO ambaye ni mwenyekiti wao ikiwataka wabadilike na kujitathmini na sisi tungependa tuone mabadiliko hayo ndani ya wiki mbili” amesema

Akizungumza kwa niaba ya waganga wakuu wa Halmashari za mkoa wa Ruvuma Dkt. Mussa Rashid,Mganga mkuu wa Halmashauri ya wilaya ya Madaba mkoa wa Ruvuma amekiri kupokea maelekezo hayo kutoka Ofisi ya Rais-TAMISEMI na amewaomba wataalamu wa sekta ya Afya kubadilika na kuwajibika katika taaluma zao ili mwananchi apate huduma stahiki.

“Kuna kitu tumefungua katika akili zetu kwamba ‘we need to practise as profesional’ tuna eneo hilo embalo tumekuwa tukijiweka nyuma na hiki nimeona umekisisitiza tangu tumeanza ziara kwamba sisi kama CHMTs na RHMTs hatutakiwi kubaki nyuma takati wa ujenzi wa miundombinu hata kidogo” amesema Dkt. Rashid

Timu ya Afya,Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka Ofisi ya Rais – TAMISEMI ikiongozwa na mkurugenzi Dkt. Rashid Mfaume ipo mkoa wa Ruvuma kwaajili ya usimamizi shirikishi na ufuatiliaji wa utoaji wa huduma za Afya katika Halmashauri za Mkoa huo.

About the author

mzalendo