Featured Kitaifa

MHE.JENISTA NA TIMU YA USIMAMIZI SHIRIKISHI TAMISEMI WAKAGUA SHUGHULI ZA AFYA PERAMIHO

Written by mzalendo

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama amesema Serikali kupitia Ofisi ya Rais TAMISEMI imejipanga kuboresha huduma za afya ili kuokoa vifo vya wakinamama na watoto wakati wa uzazi.

Mhe. Mhagama ametoa kauli hiyo wakati wa ziara katika kituo cha Afya kata ya Liganga jimbo la Peramiho Halmashauri ya wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma akiwa ameambatana na Timu ya Afya Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka Ofisi ya Rais – TAMISEMI ikiongozwa na Dkt. Rashid Mfaume iliyoko mkoa wa Ruvuma kwaajili ya Ziara ya Usimamizi Shirikishi katika maeneo ya kutolea huduma za Afya.

“Kituo cha afya Liganga kimepata vifaa tiba vya thamani ya shilingi Milioni mia tatu na hivyo kusaidia kuanza kutoa huduma za mabara na kupunguza adha ya wananchi kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya.” Amesema

Kwa upande wake Dkt. Rashid Mfaume Mkurugenzi wa hlHuduma za Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI amemshukuru Waziri Mhagama kwa kuendelea kuwatumikia wananchi wa Jimbo la Peramiho.

“Jitihada za Mbunge kuomba vituo vya afya vifaa tiba na hospitali zimesaidia sana kuboresha huduma za afya jimbo la Peramiho ambapo kwa mwaka uliopita wa fedha nyingi zilikuja Halmashauri ya Wilaya ya Songea na zoezi la kukabidhi vifaa tiba ni ishara tosha kwamba kituo cha afya Liganga kitatoa huduma zote zinazopaswa kuwepo.”amesema Dkt. Mfaume.

About the author

mzalendo