Featured Kitaifa

KAMATI YA GEF YAKOSHWA UTEKELEZAJI PROGRAMU KIZAZI CHENYE USAWA CHAMWINO

Written by mzalendoeditor

Na WMJJWM- Dodoma

Kamati ya Kitaifa ya Ushauri kuhusu utekelezaji wa Programu ya Kizazi chenye Usawa imeridhika na utekelezaji wa Programu hiyo Wilayani Chamwino hasa katika kuwezesha jamii kwenye malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto ili Mama apate muda wa kuendelea shughuli za kiuchumi.

Hayo yamebainika Julai 09, 2024 wakati wa siku ya pili ya ziara ya Kamati hiyo mkoani Dodoma yenye lengo la kufuatilia utekelezaji wa Programu hiyo.

Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati hiyo Nangi Masawe amesema uwepo wa Vituo vya Malezi na Makuzi inatoa fursa kwa Wanawake kuendeleza shughuli zao za kiuchumi kwani wakikosa sehemu sahihi za kuwaacha watoto wao wanaweza kupatwa na madhira ya ukatili na wao pia kukosa fursa mbalimbali za kupata kipato na kufikia Usawa wa kijinsia katika uchumi.

Ameongeza kuwa lengo kubwa la Programu ya Kizazi chenye Usawa sio kumwezesha mwanamke kifedha tu kupata mtaji wa biashara bali kuweka mazingira wezeshi ya kumpunguzia adha katika sekta mbalimbali zikiwemo upatikanaji wa maji, Nishati ya umeme, Nishati safi ya kupikia na uwezeshaji katika elimu itakayomsaidia kuelekea katika Kizazi chenye Usawa nchini.

“Jambo mnalofanya hapa Walezi wa kituo hiki ni la heri sana na hii ni dhana nzuri katika kuwasaidia watoto wetu katika malezi na pia kutoa fursa kwa Wanawake kuendelea na shughuli za kiuchumi ili tuweze kufika Kizazi chenye Usawa kama Mhe. Rais alivyoweka ahadi Kimataifa” alisisitiza Nangi

Naye Mjumbe wa Kamati hiyo Carolyn Kandusi amesema kuwepo wa vituo vya Malezi sio inampunguzia mzazi mzigo wa malezi kwa Mtoto na kukosa muda wa Kufanya shughuli za kiuchumi bali inasaidia watoto kupata Malezi stahili wakiwa katika vituo husika, hivyo itasaidia kujenga familia, Jamii na Taifa lenye imara katika malezi kwa watoto.

“Nimefurahishwa sana kuona juhudi za Wilaya hii ya Chamwino katika kuhakikisha inawasaidia Wanawake kupata sehemu sahihi za kuwaacha watoto wao wakipata Malezi na wao kufanya shughuli zingine za kiuchumi, Sisi kama Kamati tutamshauri Mhe. Rais Vituo hivi viweze kuwepo katika Shule zote za Msingi ili kusaidia Jamii” amesema Carolyn

Akielezea Programu ya Kizazi chenye Usawa wakati wa ziara hiyo Mratibu wa Programu hiyo kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Leah Ipini amesema kuwa Programu hiyo inalenga kuleta haki na usawa kwa wanawake na wanaume hivyo itapelekea kupungua kwa vitendo vya ukatili, fursa sawa katika matumizi ya Teknolojia, uhuru na haki kwa Wanawake, uwekezaji wenye mlengo ya kijinsia, matumizi ya Nishati safi, upatikanaji wa maji safi na salama karibu na kutatua changamoto mbalimbali zilizokuwa zinamfanya mwanamke akose muda mwingi wa kufanya shughuli za kiuchumi na kujiletea maendeleo.

Naye mmoja ya mzazi wanaufaika kwa Kituo cha Malezi na Makuzi ya Awali ya Mtoto katika Shule ya Msingi Chamwino Agness Joram ameishukuru Serikali kwa kuwezesha upatikanaji wa vituo hivyo katika maeneo yao kwani vinawasaidia kupata muda wa kufanya shughuli zao za kiuchumi na kuwapa watoto wao Malezi ya Awali wanayostahili.

About the author

mzalendoeditor