Featured Kitaifa

MAJIMBO YOTE YA UCHAGUZI MKOA WA MWANZA KUPATA BARABARA ZA KIWANGO CHA LAMI-MHANDISI AMBROSE

Written by mzalendo

Katika kipindi cha mwaka 2023/2024 serikali imetekeleza miradi 7 ya maendeleo katika mkoa wa Mwanza yenye urefu wa kilomita 39 ambapo gharama za miradi hiyo ni Shilingi Bilioni 56.038 ambapo majimbo yote ya uchaguzi yatapata barabara ya lami.

Akizungumza mara baada ya kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya ujenzi wa barabara ili kujionea hatua zilizofikiwa za ujenzi, Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania-TANROADS Mkoa wa Mwanza Mhandisi Paschal Ambrose ameitaja miradi hiyo ambayo ni pamoja na mradi wa Ujenzi wa kilomita 10 za kiwango cha lami katika barabara ya Isandula (Magu)- Hungumalwa kwa gharama ya Shilingi Bilioni 14.099 ambapo Mkandarasi ameanza hatua za awali za kupeleka vifaa na mitambo eneo la mradi.

Ameutaja mradi mwingine kuwa ni Ujenzi wa kilomita 3.0 za barabara ya Mabuki- Jojiro- Ngudu yenye gharama ya shilingi Bilioni 3.495 ambapo Mkandarasi anaendelea na kazi ya kusafisha ushoroba wa barabara ambapo kwa ujumla maendeleo ya Mradi ni asilimia 10.

Amesema kuwa jumla ya Bilioni 18.406 zinatarajiwa kutumika kwa ajili ya Ujenzi wa kilomita 10.0 za barabara ya Mwanza Airport – Kayenze – Nyanguge kwa kiwango cha lami ambapo tayari Mkandarasi ameanza hatua za awali za kupeleka vifaa na mitambo eneo la mradi.

Mradi mwingine ni wa Ujenzi wa kilomita 3.0 za barabara ya Bukokwa – Nyakalilo kwa kiwango cha lami ambayo kwa sasa Mkandarasi anaendelea na kazi ya kusafisha ushoroba wa barabara huku Mradi huo ukiwa umefikia asilimia 10 kwa gharama ya Shilingi Bilioni 3.402.

Mhandisi Ambrose amesema pia serikali imetenga Shilingi Bilioni 9.206 kwa ajili ya ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilomita 7.0 kwa kiwango cha lami kuanzia Nansio mpaka Rugezi ambapo hadi hivi sasa Mkandarasi anaendelea na kazi ya kusafisha ushoroba wa barabara.

Vilevile amesema kuwa TANROADS inatarajia kutumia shilingi Bilioni 3.898 kwa ajili ya Ujenzi wa kilomita 3.0 kwa kiwango cha lami kwenye barabara ya Mwanangwa – Misasi- Salawe- Kahama ambayo kwa sasa Mkandarasi anaendelea na kazi ya kusafisha ushoroba wa barabara na uwekaji wa moramu kwa ajili ya tabaka za chini za barabara ambapo kwa ujumla maendeleo ya Mradi umefikia asilimia 15.

Hali kadhalika serikali inatarajia kutumia kiasi cha shilingi Bilioni 3.529 kwa ajili ya Ujenzi wa barabara ya Kamanga – katunguru- sengerema kwa kiwango cha lami ambapo kwa sasa Mkandarasi anaendelea na kazi za ujenzi wa makalavati, maboksi kalavati pamoja na matabaka ya chini ya barabara (G7 & G15) ambapo kwa ujumla maendeleo ya Mradi ni asilimia 40.

Mhandisi Ambrose ameishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha hizo ambazo zimetumika kuimarisha miundombinu nchini kwa ajili ya kuchochea uchumi wa wananchi.

Amemshukuru pia Waziri wa Ujenzi Mhe Innocent Bashungwa, Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Balozi, Mhandisi Aisha Amour, Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania -TANROADS Mhandisi Mohamed Besta kwa kazi kubwa na nzuri ya usimamizi wa sekta ya ujenzi kwani miundombinu mingi imeendelea kukamilishwa.

Amewasihi wananchi kuendelea kuzitunza na kuzilinda barabara hizo ili ziweze kuleta tija katika jamii itaishi muda mrefu na serikali kuendelea kuwekeza katika maeneo mengine badala ya kuendelea kukarabati barabra moja.

About the author

mzalendo