Tume ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa imetangaza kuwa, imeguswa na ripoti za kuongezeka mauaji dhidi ya raia nchini Burkina Faso.
Tume ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa inaeleza hayo huku taarifa zikionyesha juu ya kuhusika jeshi na mamluki wa kigeni katika mauaji hayo.
Kamishna Mkuu wa tume hiyo Volker Turk amesema, licha ya makundi yenye silaha kuhusishwa na idadi kubwa ya mauaji, inasikitisha kuwa vikosi vya usalama pia vinatekeleza mauaji hayo kiholela.
Turk ametoa wito kwa mamlaka nchini humo kuhakikisha raia wanalindwa, wakati huu makundi ya kujihami yakiendeleza mashambulio dhidi ya raia ikiwemo wakimbizi wa ndani.
Aidha, ametoa wito kwa Serikali ya Rais Ibrahim Traore kuunga mkono uchunguzi huru na wa uwazi kuhusu tuhuma zote za ukiukaji wa haki za kibinadamu, na kuhakikisha kuwa wahalifu wanafikishwa mahakamani.
Hivi karibuni serikali ya Burkina Faso ilikanusha vikali na kulaani tuhuma zilizotolewa na shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch ambalo lililituhumu jeshi la serikali ya nchi hiyo kuwa lilihusika na mauaji ya mwezi Februari mwaka huu 2024 katika vijiji vya Nodin na Soro kaskazini mwa nchi hiyo.
Serikali ya Burkina Faso inasema kuwa, kampeni inayoenezwa na vyombo vya habari kuhusu tuhuma dhidi ya serikali ya nchi hiyo inaonyesha kikamilifu nia mbaya yenye lengo la kushusha hadi ya jeshi la Burkina Faso.
#Chanzo cha habari hii ni Parstoday Afrika.