Na Gideon Gregory, Dodoma.
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amesema Wizara hiyo ina mpango wa kufunga mizani yenye
teknolojia inayopima uzito wa magari yakiwa kwenye mwendo (Weigh in Motion System), katika vituo vyote vya mizani nchini ili kutatua changamoto ya msongamano wa magari katika vituo vya mizani.
Waziri Bashungwa ameyasema hayo leo Mei 29,2024 Bungeni Jijini Dodoma wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha ujao 2024/25 na kuongeza kuwa katika mwaka huo mizani 32 itajengwa lengo likiwa ni kuwa na jumla ya mizani 110 ifikapo mwaka 2026/27.
“Mizani hii yenye teknolojia ya kisasa hufungwa
barabarani ili kuchuja magari ambayo hayajazidi uzito na kuyaruhusu kuendelea na safari, hivyo msafirishaji hatalazimika kuingia katika kituo cha mzani endapo gari lake halitabainika kuzidi uzito katika mizani ya WIM”,amesema.
Amesema Mizani ya aina hiyo itasaidia kwa sehemu kubwa kupunguza msongamano wa magari barabarani na katika vituo vya mizani, kupunguza muda wa safari kwa magari yaliyobeba mizigo inayokwenda nje ya nchi (Transit Vehicles) na ndani ya nchi, na hivyo kuendelea kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi.