Featured Kitaifa

POLISI WILAYANI MISSENYI WATAKIWA KUWA MABALOZI WA ELIMU YA FEDHA

Written by mzalendo

Mkuu wa Polisi Wilaya ya Missenyi SP. Jonas Sira Soa, akiteta jambo na Afisa Usimamizi wa Fedha Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha Bi. Mary Mihigo na Afisa Usimamizi wa Fedha Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha Bw. Stanley Kibakaya, baada ya kumalizika kwa semina iliyotolewa na Wizara ya Fedha kuhusu elimu ya fedha kupitia mada mbalimbali ikiwemo kujiwekea akiba, masuala ya akiba kwa Polisi, wilayani Missenyi.

Afisa Mwandamizi Uchambuzi wa Masuala ya Fedha kutoka Mamlaka ya Masoko na Mitaji na Dhamana (CMSA) Bi. Gladness Mollel, ekieleza kuhusu faida za uwekezaji kwa Polisi walioshiriki semina ya elimu ya fedha iliyotolewa na Wizara ya Fedha ambayo ilihusisha mada mbalimbali ikiwemo kujiwekea akiba, masuala ya uwekezaji, wilayani Missenyi.

Mkuu wa Polisi Wilaya ya Missenyi SP. Jonas Sira Soa, akiteta jambo na Afisa Usimamizi wa Fedha Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha, Bw. Stanley Kibakaya, wakati wa semina iliyotolewa na Wizara ya Fedha kuhusu elimu ya fedha kupitia mada mbalimbali ikiwemo kujiwekea akiba, masuala ya akiba kwa polisi, wilayani Missenyi.

Mkuu wa Kituo cha Polisi Kyaka, wilayani Missenyi OCS. Emmanuel Wandwi, akizungumza wakati wa kikao, kilichowahusisha Timu ya Wataalamu wa Wizara ya Fedha na Polisi ambapo walipata fursa ya kupewa elimu ya masuala mbalimbali ya fedha ikiwemo kujiwekea akiba, kwa Polisi, wilayani Missenyi.

Baadhi ya Polisi wa Wilaya ya Missenyi walioshiriki semina ya elimu ya fedha wakifuatilia maelezo ya mada mbalimbali ikiwemo utunzaji wa akiba na mikopo iliyofanyika katika Viwanja vya Kituo Cha Polisi Kyaka, Wilaya ya Missenyi mkoani Kagera.

Mkaguzi wa Polisi Bw. Baraka Mafwimbo, akichangia jambo wakati wa kikao kilichowahusisha Timu ya Wataalamu wa Wizara ya Fedha na Polisi ambapo Polisi hao walipata fursa ya kupewa elimu ya masuala mbalimbali ya fedha ikiwemo kujiwekea akiba, kwa Polisi, wilayani Missenyi, mkoani Kagera.

Baadhi ya Polisi wa Wilaya ya Missenyi walioshiriki semina ya elimu ya fedha wakifuatilia maelezo kupitia mada mbalimbali zilizofundishwa ikiwemo utunzaji wa akiba na mikopo iliyofanyika katika Viwanja vya Kituo Cha Polisi Kyaka, Wilaya ya Missenyi mkoani Kagera.

Mkuu wa Polisi Wilaya ya Missenyi SP. Jonas Sira Soa (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Timu ya Wataalamu wa Wizara ya Fedha baada ya kumalizika kwa semina iliyotolewa na Wizara ya Fedha kuhusu elimu ya fedha ambapo mada mbalimbali zilifundishwa ikiwemo kujiwekea akiba, wilayani Missenyi. Kushoto ni Mkuu wa Kituo cha Polisi Kyaka, wilayani Missenyi OCS. Emmanuel Wandwi na Afisa Usimamizi wa Fedha Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha Bw. Stanley Kibakaya.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WF, Kagera)

Na: Josephine Majula, WF – Kagera

Polisi Wilayani Missenyi wametakiwa kuwa mabalozi kwa wananchi wanaowazunguka ili kuwafikishia elimu ya masuala ya fedha waliyoipata kutoka kwa Timu ya Wataalamu ya Wizara ya Fedha iliyoko katika kampeni ya kutoa elimu ya fedha kwa umma katika mikoa mbalimbali nchini.

Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Missenyi SP. Jonas Sira Soa, wakati akizungumza na Askari Polisi katika semina iliyofanyika katika Viwanja vya Kituo Cha Polisi Kyaka, Wilaya ya Missenyi, mkoani Kagera.

“Tunaahidi kuwaelimisha Polisi wengine ambao hawajapata elimu hii, lakini pia tutawajengea uwezo Polisi Jamii ili wawaelimisha wananchi ambao wapo karibu nao ili waepukanane na mikopo umiza”, alisema SP Soa.

Alisema kuwa elimu ikiwafikia wananchi wote nchini itaisaidia Serikali kupondokana na kupunguza migogoro ya kesi mbalimbali zinazoendelea kwenye Vituo vya Polisi kuhusu mikopo inayowakumba wananchi mbalimbali.

Naye Mkaguzi wa Polisi Baraka Mafwimbo, aliiomba Serikali kuongeza nguvu ya kudhibiti na kuimarisha mifumo ya Taasisi zinazohusika na utunzaji wa taarifa binafsi za wananchi kuhakikisha zinalinda taarifa hizo ili kuepusha taarifa hizo kufikiwa na watoa huduma ya mikopo na kuweza kuwashawishi kukopa fedha.

“Binafsi nimewahi kupigiwa simu na kushawishiwa kuchukua mkopo na watoa huduma ambao sikujua taarifa zangu wamezitoa wapi, lakini walikuwa wananielezea kama wananifahamu lakini hawakuweza kufanikiwa kwa kuwa nimewahi kupata elimu ya masuala ya fedha zamani’. Alisema Mafwimbo.

Kwa upande wake Afisa Usimamizi wa Fedha Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha, Bi. Mary Mihigo, aliwasisitiza wananchi na polisi kuhakikisha wanatumia kuomba mikopo kwenye Taasisi za Fedha zilizosajiliwa rasmi ili kujiepusha na matapeli.

“Utajua kuwa ni Taasisi rasmi ya kukopesha, kupitia Tovuti ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ambayo imeorodhesha Taasisi rasmi zote za utoaji mikopo nchini hivyo ni lazima mwananchi kabla hajakopa kujiridhisha kwenye usajili wa Taasisi husika”, alisema Bi. Mihigo.

Alisema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Fedha, itaendelea kutoa elimu ya masuala fedha kwa wananchi wa makundi mbalimbali ili kuhakikisha wananchi wanakuwa na uelewa mpana wa masuala ya fedha ikiwemo elimu ya mikataba, uwekezaji na mikopo umiza.

About the author

mzalendo