Featured Kitaifa

MAKAMU WA RAIS KUZINDUA MBIO ZA MWENGE APRIL 2,2022 NJOMBE

Written by mzalendoeditor

NAIBU Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu,Kazi,Ajira na Vijana,Patrobas Katambi,kizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) leo Machi 29,2022 jijini Dodoma  kuhusu uzinduzi wa mbio za Mwenge utakaozinduliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dk.Philip Mpango Aprili 2,2022  katika uwanja wa Sabasaba Mkoani Njombe ambapo kilele chake kinatarajiwa kuwa Mkoani Kagera Oktoba 14 mwaka huu.

……………………………………………………

Na Alex Sonna-DODOMA

NAIBU Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu,Kazi,Ajira na Vijana,Patrobas Katambi,amesema kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dk.Philip Mpango anatarajiwa kuzindua mbio za mwenge Aprili 2,2022  katika uwanja wa Sabasaba Mkoani Njombe ambapo kilele chake kinatarajiwa kuwa Mkoani Kagera Oktoba 14 mwaka huu.

Katambi ameyasema hayo leo Machi 29,2022 jijini Dodoma wakati kizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu uzinduzi wa mbio hizo  kwa mwaka 2022.

 Katambi amesema baada ya uzinduzi huo, vijana  sita waliondaliwa kutoka Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar, watabidhiwa jukumu la kuukimbiza  katika Mikoa 31 na Halmashauri 195 za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa siku 195.

“Kwa kipindi hiki chote, Mwenge wa Uhuru utafanya kazi ya kuhamasisha amani, umoja, upendo na Mshikamano wa Kitaifa, Kushiriki shughuli za Maendeleo katika maeneo yao,”amesema.

Amesema ujumbe wa mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu umezingatia, hoja, na vipaumbele vya Serikali ya awamu ya sita vyenye dhamira ya kuhakikisha Tanzania inakuwa miongoni mwa nchi zenye uchumi wa juu wa kati ifikapo mwaka 2025.

“Hivyo, Ujumbe mkuu unasititiza juu ya umuhimu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 “ Sensa ni Msingi wa Mipango ya Maendeleo: Shiriki kuhesabiwa, tuyafikie Maendeleo ya Taifa ”.

“Pamoja na Kauli Mbiu hii, Mbio za Mwenge wa Uhuru zitaendelea kuelimisha na kuihamasisha jamii ya Watanzania kuhusu umuhimu na uzingatiaji wa Lishe bora, Mapambano dhidi ya Rushwa, Mapambano dhidi ya VVU/UKIMWI, Mapambano dhidi ya matumizi ya Dawa za kulevya,”amesema.

Aidha Katambi amesema mbio hizo  zimekuwa zikitumika kuelimisha wananchi katika maeneo yote nchini juu ya masuala ya kisekta na kisera katika muktadha wa Kitaifa na Kimataifa.

“Ikiwa ni pamoja na kuendeleza juhudi za kupambana na maradhi yanayotishia ustawi wa watu wetu kama vile UKIMWI, Malaria, UVIKO -19 na kupambana na matumizi ya Dawa za kulevya na Vitendo vya Rushwa,”amesema.

Aidha,Mwenge wa Uhuru umeendelea kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa lishe bora kwa afya imara.

“Pamoja na njia nyingine tunazotumika kuwahamasisha wananchi wetu, bado Mbio za Mwenge wa Uhuru zimekuwa ni njia sahihi ya kufikisha taarifa na elimu sahihi ya kutatua changomoto kwa watanzania,”amesema.

Vilevile,mbio hizo  zimeendelea kuhamasisha na kuimarisha Muungano  kwa pande zote mbili za nchi yetu.

Amesema mwenge huo umekuwa na  falsafa ya kumulika ndani na nje ya mipaka ya Taifa  kwa kumulika uovu katika jamii ikiwemo uzembe, kutowajibika, vitendo vya rushwa na ufisadi katika miradi mbalimbali ya maendeleo na huduma za kijamii nchini.

“Na kimefanya kazi ya kuratibu na kutathimini shughuli mbambali za maendeleo zinazofanywa na wadau wa maendeleo,”amesema.

 Katambi amesema kwa kipindi cha tangu nchi yetu ipate uhuru hadi mwaka1992, Mbio za Mwenge wa uhuru zilikuwa zikisimamiwa na kuratibiwa na Chama Tawala kupitia umoja wa Vijana.

“Baada ya nchi yetu kuingia mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992;Mbio za Mwenge wa Uhuru zilianza kusimamiwa na Serikali chini ya Wizara zenye dhamana na Maendeleo ya Vijana.

“Uamuzi huu ulilenga kuwakilisha wananchi wote bila kujali itikadi zao za Kisiasa, Dini, Rangi na Ukabila. Huu ni mwaka 30 tangu Serikali ianze kuratibu na kusimamia mbio hizi,”amesema.

About the author

mzalendoeditor