Featured Kitaifa

TAMISEMI WAKUTANA NA SHIRIKA LA GOOD NEIGHBORS TANZANIA

Written by mzalendo

Na OR TAMISEMI, DODOMA

Mkurugenzi wa Idara ya Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii Ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt. Rashid Mfaume amefanya mazungumzo na Shirika la Good neighbors Tanzania ambapo amewaasa kuendeleza mambo mazuri wanayoyafanya kupitia kazi zao hapa nchini.

Dkt. Mfaume amewapongeza Shirika la Good neighbors ofisini kwake Jijini Dodoma leo tarehe 24.05.2024 kwa kusema kazi zinazoleta tija katika jamii mfano mzuri kwa Wadau wanaoshirikiana na Serikali kwani wadau hao kwa mkoa wa Mwanza pekee wamejenga tenki la maji lenye uwezo wa kuhifadhi lita 50,000, ujenzi wa zahanati na uwekaji wa vifaa tiba, kutibu magonjwa na kutoa dawa kwa kushirikiana na Serikali.

Katika mazungumzo na Ofisi ya Rais TAMISEMI Bw. Dominic Mbamba Meneja Operesheni Shirika la Good neighbors amesema shirika lake limeweza kuwasiliha kazi zake inazofanya katika mikoa ya Dodoma, Dar es Salaam, Pwani, Mwanza, Kigoma na Songwe lengo likiwa ni kujenga mahusiano mazuri na Serikali, kufanya kazi pamoja katika Sekta wanazozifanyia kazi ili kufikia malengo waliyojiwekea kwa manufaa ya watanzania.

Bw. Mbamba ameongeza kuwa shirika hilo la Kimaifa linajihusisha na masuala la Kilimo Tija, Afya na Lishe, Elimu, huduma za maji (water sanitation and hygiene) na masuala ya kujiongezea kipato kwa jamii.

Amesema kazi zilizofanywa na Shirika ni pamoja na kujenga zahanati na kuweka vifaa tiba, kuwafundisha walimu njia za kufundishia na ufaraguaji wa zana ili kuboresha eneo la ufundishaji kwa wanafunzi, kutoa mafunzo ya kilimo kwa wakulima na kuwapatia mbegu bora ili kujiongezea kipato na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kujenga vituo vya utayari kwa ajili ya watoto ambao hawajaanza shule za msingi ili waweze kujifunza na kujipatia elimu.

Aidha, Bw. Mbamba amesema mkoani Mwanza katika visiwa vya Kome na Chifunfu wameweza kutoa huduma za magonjwa yasiyopewa kipaumbele ambayo ni kichocho na minyoo kwa kutoa dawa na tiba, ujenzi wa zahanati, ujenzi wa kituo cha utafiti wa magonjwa, kujenga miundombinu mizuri ya maji safi na salama na kutoa elimu kwa jamii kujikinga na magonjwa.

Amesema Shirika hilo katika mikoa ya Pwani na Dar es Salaam wameweza kutoa elimu ya ufundi wa kisasa kama vile utengenezaji wa mfano wa taa za barabarani, magari, na mifumo ya maji ya umwagiliaji ( STEAM) kwa ajili ya kukuza uwezo wa teknolojia kwa watoto lakini pia wamejenga shule za sekondari za Maendeleo na Fokayosi ili kuboresha mazingira ya ujifunzaji kwa wanafunzi.

Aidha, wameweza kuwalipia Bima ya Afya watoto wapatao 7000 waliopo kwenye mazingira magumu katika mikoa ya Dodoma, Dar es Salaam, Pwani, Mwanza, Kigoma na Songwe.

About the author

mzalendo