Featured Kitaifa

MBUNGE AIPONGEZA TAASISI YA MAMA ONGEA NA MWANAO BUNGENI KWA KUGAWA VIATU KWA WANAFUNZI

Written by mzalendoeditor
Na Mwandishi Wetu
 
MBUNGE wa Viti MAALUM Mkoa wa Kilimanjaro Mhe Esther Maleko ameipongeza Taasisi ya Mama Ongea na Mwanao kwa mchango wao mkubwa wa kusaidia jamii kwa kugawa viatu kwa wanafunzi kupitia Kampeni Samia Nivishe Kiatu.
 
Amesema kupitia Kampeni hiyo ya Samia Nivishe Kiatu imefanya wanafunzi au Wazazi wasiokuwa na uwezo wa kununua viatu kupata viatu kutoka kwa Mama Ongea na Mwanao.
 
Akizungumza Bungeni Mjini Dodoma Mbunge Maleko amelieleza Bunge Taasisi ya Mama Ongea na Mwanao inayoongozwa na Mwenyekiti wake Stiven Nyerere,Katibu Monalisa pamoja na wasanii wengine unapaswa kuungwa mkono.
 
Amesema mikopo inayotolewa kwa wasanii iko haja ya kuangalia namna ya kuiwezesha Taasisi ya Mama Ongea na Mwanao ili iweze kupata fedha kwa ajili ya kutekeleza majukumu yake ya kuendelea kuwafikia wanafunzi walioko maeneo mbalimbali nchini.
 
“Napenda kuwapongeza Mama Ongea na Mwanao ,wasanii hawa wakiongozwa na Mwenyekiti wao Steven Nyerere,Katibu wao Monalisa pamoja na wanachama wote wamefanya kazi kubwa sana kwa kuwafikia Watanzania
 
“Tumeona wamekuja na viatu vya mama Samia ,Mama Samia nivishe kiatu ,wamewafikia watoto ambao hawana fedha au wazazi wao hawana fedha ya kuwanunulia wanafunzi hao viatu kwa ajili ya kwenda shule
 
“Hili ni jambo kubwa la kujivunia lakini sio hivyo tu wamekuja pia na baiskeli ya Mama Samia Suluhu Hassan.Jamani baiskeli hii inakwenda kuwasaidia wale watoto wenye ulemavu nao waweze kwenda shuleni bila usumbufu wowote.Tunapongeza sana hawa wa Mama Ongea na Mwanao wanajituma sana,”amesema.
 
Ameongeza kwamba “Naibu Spika nashauri Wizara ione namna gani katika ile mikopo ya wasanii vijana hawa waweze kupewa fedha ziweze kutekeleza majukumu yao.”

About the author

mzalendoeditor