Featured Kitaifa

DARAJA LA RUHEMBE LAWAFUTUTA MACHOZI WANANCHI WA MIKUMI

Written by mzalendo

Kwa muda mrefu wananchi wa Kata za Ruhembe, Kidodi, Uwembe, Vidunda, Mikumi na Kilolo wameteseka kwa kusafiri umbali mrefu au kuzunguka kwenye mapori ya miwa kufikia huduma za kijamii.

Hali hiyo ilitokana na kukosekana kwa kiunganishi madhuhuti cha miundombu ya barabara katika kata hizo.

Akizungumza wakati wa ziara ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mohamed
Mchengewa, Mbunge wa Jimbo la Mikumi Mhe. Denis Londo amesema wananchi hao walitumia gharama kubwa katika kuzalisha mazao yao.

“Kukosekana kwa daraja, kulichangia gharama kubwa ya uzalishaji wa mazao kwa mkulima kutokana na kuwapo ugumu wa upatikanaji wa mbegu na pembejeo.”
“Hadi mkulima anakuja kuuza mazao yale hapati faida kwa kuwa ametumia gharama kubwa wakati wa kupanda na kukuza mazao yake kutokana na kukosekana kwa miundombinu rafiki.”

Londo ameishukuru Serikali kwa ujenzi wa Daraja la Luhembe ambalo kwa kiasi kikubwa litampunguzia mkulima gharama za uzalishaji.

Akizungumza katika ziara hiyo Meneja wa TARURA Mkoa wa Morogoro Eng. Emmanuel Ndyamkama amesema daraja hilo litakua na urefu wa mita 40 na litagharimu takribani Sh bilioni 1.2.

Akitoa maelekezo wakati wa ziara hiyo, Mhe Mchengerwa aliwataka TARURA Mkoa wa Morogoro kuhakikisha ujenzi wa daraja hilo unakamilika kwa wakati na kuwataka kujenga barabara za lami zenye urefu wa mita 100 kwa kila upande kuunganisha daraja hilo.

“Nimeona ujenzi unaendelea vizuri sasa na mmeniambia kuwa mmepanga kujenga barabara za kuunganisha daraja hilo zenye urefu wa mita 15 sasa niwatake muongeze zifikie mita 100 kila upande.”

“Pia ongezeni kuweka na taa za barabara kumi kwa pande za kuingilia na kutokea kwenye daraja ili kuwe na mwanga wakati wote.”

Mhe Mchengerwa alisema katika kuzuia mmomonyoko katika eneo hlinalojengwa daraja ameitaka TARURA kuweka ‘Gabions’ za kutosha.

Mhe. Mchengerwa yuko katika ziara ya kizi mkoani Morogoro na ameshatembelea Halmashauri za Wilaya ya Kilosa na Ifakara Mji.

About the author

mzalendo