Featured Kitaifa

MSOMERA WAMSHKURU RAIS SAMIA

Written by mzalendo

Wakazi wa Kijiji cha Msomera, Wilaya ya Handeni mkoani Tanga wamemshkuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dk. Samia Suluhu Hassan kwa maendeleo mbalimbali na uboreshwaji wa huduma katika kijiji hicho.

Kwa nyakati tofauti, wakazi hao wamesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais, Dk. Samia imefanya maendeleo makubwa katika kijiji chao toka walivyohama kutoka Ngorongoro huku wakibainisha baadhi ya manufaa waliyoyapata ni pamoja na kupatiwa nyumba, kuweka umeme, kujengewa zahanati na hospitali.

Wanakijiji hao wametoa shukrani hizo jana Mei 17 wakati wa hafla ya kukabidhiwa nishati safi za kupikia yakiwamo majiko banifu na majiko ya gesi iliyoongozwa na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga.

Wakati wa hafla hiyo, Naibu Waziri Kapinga amewataka wanakijiji hao pamoja na Watanzania kwa ujumla kuacha mazoea ya kutumia kuni na mkaa kupikia na badala yake watumie nishati safi za kupikia ili kutunza afya zao na mazingira kwa ujumla.

Naibu Waziri Kapinga amesema kuwa ugawaji wa majiko hayo ni miongoni mwa mipango na mikakati ya serikali kuhakikisha ifikapo 2034, asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia.

          

About the author

mzalendo