Featured Kitaifa

SEKTA BINAFSI KUUNGA MKONO BAJETI YA MWAKA 2024/25

Written by mzalendo
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye, akizungumza Bungeni jijini Dodoma, wakati akiwasilisha bajeti ya wizara hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2024/ 2025.
Na Mwandishi wetu, WHMTH. 
Sekta binafsi imeendelea kuunga mkono jitihada za Serikali katika maendeleo ya sekta ya habari, mawasiliano na teknolojia ya habari, katika utekelezaji wa Bajeti ya Mwaka 2024/25. 
Hayo yamesemwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye, Bungeni jijini Dodoma, wakati akiwasilisha hotuba ya Bajeti ya wizara yake, na kuelezea mchango wa sekta binafsi katika utekelezaji wa Bajeti ya Mwaka 2024/25.
Waziri Nape amesema, katika kuunga mkono jitihada hizo za Serikali, sekta binafsi imeridhia kutekeleza mambo kadhaa, ikiwemo ujenzi wa minara ya mawasiliano ya simu.
Amesema tayari kampuni za simu za Airtel Tanzania, Vodacom Tanzania, Honora Tanzania, Halotel na TTCL, zimepanga kuendelea kushirikiana na Serikali kwenye ujenzi wa minara 616, kati ya minara 758, na kuendelea kuongeza uwezo kwenye minara 61 kati ya minara 304. 
Aidha, Waziri Nape amesema, kampuni hizo pia zimepanga kushirikiana na Serikali katika ujenzi wa minara mipya 636 ya mawasiliano ya simu. 
Kwa upande wa Kampuni ya Simu ya Airtel Tanzania, Waziri Nape amesema, yenyewe imepanga kupeleka huduma ya Wi-Fi katika maeneo 16 kati ya 120, yaliyopendekezwa na Wizara kwa Mwaka 2024/25.
Amesema, maeneo yatakayofikishiwa huduma hiyo ni pamoja na vyuo, masoko, hospitali, vituo vya mabasi na stesheni za treni ya mwendokasi. 
Waziri Nape amesema, nayo Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika, Tawi la Tanzania (MISA-TAN, imepanga kutoa elimu kwa umma kuhusu matumizi sahihi ya huduma za mawasiliano nchini, na pia itashirikiana na Serikali, kukuza bunifu za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na kukuza kampuni changa za TEHAMA.

About the author

mzalendo