Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Bi. Ummy Mohammed Wayayu,akizungumza kuhusu mfumo wa kuwezesha uratibu wa shughuli za uandaaji wa vikao mbalimbali vya bodi na menejimenti katika Halmashauri na Taasisi za Umma. (e-Board) Ofisini kwake Ilemela jijini Mwanza.
Na.Mwandishi Wetu-MWANZA
Matumizi ya Mfumo wa kuwezesha uratibu wa shughuli za uandaaji wa vikao mbalimbali vya bodi na menejimenti katika Halmashauri na Taasisi za Umma. (e-Board), umetajwa kurahisisha uendeshaji wa vikao na kupunguza gharama za maandalizi katika halmashauri ya Manispaa ya Ilemela jijini Mwanza.
Akizungumza kuhusu mfumo huo ofisini kwake jijini Mwanza, Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Bi. Ummy Mohammed Wayayu, amesema kuwa kabla ya halmashauri hiyo kuanza kutumia mfumo wa e-Board mwaka 2023, fedha nyingi zilikuwa zinatengwa katika ununuzi wa shajara,wino na vifaa vingine kwa ajili ya vikao vya madiwani na menejimenti.
“Kwa mwaka tulikuwa tunatumia takribani shilingi milioni 200 hadi 300 katika maandalizi ya uendeshaji wa vikao, lakini kwa sasa gharama hizo hatuna tena kwakuwa tunatumia mfumo huu wa e-Board, ambao umetusaidie kupeleka fedha hizo katika mambo mengine ya muhimu katika halmashauri,” alisema Bi.Ummy.
Aliongeza kuwa, mfumo wa e-Board umesaidia kupunguza gharama za kudurufu taarifa mbalimbali na badala yake zinapakiwa kwenye mfumo na madiwani wanapakuwa na kuendelea kuzifanyia kazi.
Licha ya mfumo huo kusaidia katika kupunga gharama, Mkurugenzi huyo amesema kwamba mfumo wa e-Board umesaidia katika upigaji wa kura za siri katika uchaguzi wa Wenyeviti wa Kamati pamoja na uchaguzi wa Mstahiki Meya.
“Hapo awali usiri katika chaguzi hizo ulikuwa mdogo sana, lakini kwa sasa tunatumia mfumo hivyo kura zinakuwa za siri na kila mtu ndani ya nafsi anajua amemchagua nani,” alifafanua.
Aidha, Bi Ummy aliongeza kuwa mfumo wa e-Board unawasaidia madiwani kushiriki katika kila kikao hata wanapokuwa nje ya halmashauri hiyo kwa kutumia vishkwambi ambavyo vimewezeshwa matumizi ya mfumo huo na kugawiwa kwa kila diwani.
Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Halmashauri hiyo Mheshimiwa Renatus Mulunga, alisema kuwa mfumo wa e-Board umewasaidia madiwani kuendesha vikao vyao kwa ufanisi ili kuboresha huduma za wananchi wa Ilemela.
“Nina miaka 25 kwenye udiwani, huko nyuma ilikuwa lazima ujaze gari mafuta kwa ajili ya kusambaza makarabrasha, lakini kupitia mfumo wa e-Board kila diwani anapata taarifa na makabrasha yake popote alipo kupitia mfumo na kuanza kuyafanyia kazi,” alisema Bw. Mulunga.
Mhe.Mulunga alitoa rai kwa halmashauri nyingine ambazo bado hazijaanza kutumia mfumo wa e-Board, kufanya ziara halmashauri ya Manispaa ya ilemela ili zikajifunze au kuwasiliana na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), ili zipate uelewa kuhusu mfumo huo.
Naye Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA wa Halmashauri ya Ilemela Bw.Isaack Tanguye, alisema kwamba halmashauri hiyo ilianza kutumia mfumo wa e-Board baada ya kupata malalamiko kuhusu gharama kubwa za uandaaji wa vikao.
Alisema kwamba baada ya malalamiko hayo kuwa mengi, kitengo chake kiliamua kuwasiliana na e-GA kuomba mfumo wa e-Board, na baadaye walianza kuwajengea uwezo Madiwani pamoja na Menejimenti ya halmashauri hiyo ili kuanza kufanya vikao vyao kidijiti.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela ndiyo halmashauri ya kwanza kuanza kutumia mfumo huu wa e-board kati ya halmashauri 184 nchini, mfumo huu umesanifiwa na kutengenezwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA).